Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE AISHI NA MAITI YA KAKA YAKE...MWENYEWE ADAI NI MUNGU

Polisi mjini Kakamega nchini Kenya wamemzuilia mwanamke wa makamo kwa madai ya kuishi na maiti kinyume na sheria.

Shamim Kabere, mkazi wa Iyala, eneo bunge la Lurambi, anasemekana kuuhifadhi mwili wa Ainea Tavava, 48, ndani ya nyumba yake kwa zaidi ya siku 10.

Juhudi za wakazi kutafuta chanzo cha uvundo huo usiokuwa wa kawaida ziliwafikisha hadi kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo ambapo walilazimika kuvunja mlango wake na kukuta mwili wa mtu ukioza kitandani.

"Nzi na ndege wengi walikuwa wakizunguka nyumba ya mshukiwa iliyokuwa inanuka, jaribio letu la mara moja kubaini chanzo cha harufu hiyo lilikuwa hadi wakati nzi walianza kujaa nyumbani kwake.

"Mwili uliooza ukitoka funza ulikuwa umelala kitandani, ishara kwamba aliaga dunia muda mrefu uliopita," alisema Josephine Nawire, jirani wa mshukiwa. 

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, aliyejiita mungu huyo na mtumishi wake walihamia kijijini humo miezi michache iliyopita.

 Waliishi maisha ya siri, hawakuwahi kutangamana na wengine.


Shamim alikiri kuishi na maiti hiyo akisema ni mungu wake na aliamriwa kufungiwa ndani ya chumba hicho kwa siku nyingi ili kuombea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9. 

"Kati ya siku 14 zilizohitajika, 9 zilikiwa tayari zimekamilika. Hapo awali alikuwa amenionya dhidi ya kufungua mlango kabla ya siku zilizotajwa kuisha," alisema.

 Chifu wa eneo hilo Simon Aketch alithibitisha kisa hicho akiwaomba wakaazi kuwa watulivu huku uchunguzi kuhusu suala hilo ukianzishwa.

“Mshukiwa alitumia chumba kimoja huku mwili wa mwathiriwa ukiwa katika chumba kingine, alidai kuwa hakufahamu ulikotoka uvundo huo. 
Polisi kutoka kituo cha Kakamega wameanza uchunguzi,” alisema.

 Kwa mujibu wa sheria za Kenya, mara baada ya mtu kufariki dunia akiwa nyumbani, wale walio karibu na mwili huo wanapaswa kupiga ripoti kwa chifu, ambao huwasiliana na idara ya afya na kuanza taratibu za kisheria za kushughulikia mwili huo.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com