WAJUMBE wa Bodi ya Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA),wametembelea na kukagua mtambo unaochakata na kusambaza maji ya ziwa Victoria kutoka mkoa wa Mwanza hadi Shinyanga na Tabora kwa kutumia mtambo huo.
Wajumbe hao wa Bodi ya Maji Arusha (AUWSA) wamefanya ziara hiyo Julai 14, 2022, wakiwa wameambatana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) mhandishi Patrick Nzamba na wajumbe wa bodi ya Maji Arusha, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na Mamlaka ya Maji (KASHWASA).
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Mamlaka hiyo ya Maji Arusha (AUWSA) Dk. Jackline Mkindi, amesema wamefanya ziara katika Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Kahama ,Shinyanga (KASHWASA), ili kujifunza jinsi gani wanavyoweza kuendesha mamlaka yao na kupata matokeo chanya kama ilivyo KASHWASA.
Dk. Mkindi amesema katika ziara hiyo wamejifunza vitu vingi vizuri kutoka (KASHWASA), ambapo wao kama Bodi ya Maji Arusha (AUWSA) watakwenda kuvifanyia kazi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwenye Mamlaka hiyo ya Maji Arusha.
“Tunaipongeza KASHWASA) kwa ubunifu wao mkubwa, wakutoa maji mkoa wa Mwanza hadi Shinyanga na kusambza huduma hiyo mikoa jirani ya kiwa safi na salama, huu ni ubunifu wa hali ya juu sana ambao sisi tumejifunza,”amesema Mkindi.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Patrick Nzamba akizungumza na wajumbe wa bodi ya maji kutoka AUWSA ameeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 2009 ilikuwa ni kutatua changamoto ya maji katika mji wa Shinyanga na Kahama lakini hivi sasa miji mingi inahitaji maji hayo kama vile (MwanzaNgudu,Shinyanga na Tabora) baadaye Isaka,Kishapu,Kagongwa,Igunga na Tabora.
Amesema wao ni wazalishaji wa maji wala siyo wasambazaji kwani kazi ya kusambaza maji kwa mteja mmoja mmoja inafanywa na mamlaka za maji katika miji husika kama vile KUWASA NA SHUWASA ambao ndiyo wateja wakubwa wa maji pamoja na kamati za maji za vijiji
Hata hivyo Mhandisi Nzamba amesema katika ziara hiyo imekuwa na mafanikio pia kwao, ambapo wamebadilishana mawazo na kupeana ushauri wa kiutendaji kazi hali itakayo saidia kuboresha utendaji kazi wa KASHWASA katika mkoa wa Shinyanga.
Social Plugin