Aweso amechukua hatua hiyo wakati akifungua kikao kazi kwa ajili ya maandalizi ya manunuzi ya mamlaka hiyo kwa mwaka 2022/2023 kinachofanyika mkoani Kigoma kikihusisha mameneja wa mikoa, wahasibu na maafisa manunuzi wa mikoa wa mamlaka hiyo nchi nzima.
Alisema kuwa hapendi tabia ya kuwatumbua watumishi lakini huyo amemvumilia lakini imefika mwisho na kwamba tabia ya ulevi ambayo haileti tija kwenye utendaji ndiyo sababu ya kuchukua hatua hiyo.
Waziri huyo wa maji alisema kuwa mtumishi akifanya vizuri lazima apewe zawadi na anayefanya vibaya na kuharibu kazi lazima awajibishwe.
Amewaonya watumishi wa mamlaka hiyo na kutaka wajitofautishe na watumishi wengine kwani mamlaka hiyo imeundwa kwa mkakati maalum hivyo dhamira ya kuundwa kwake lazima itekelezwe kwa vitendo.
Katika mkutano huo Waziri Aweso aliwapa zawadi za fedha watumishi watano wa RUWASA wakiongozwa na Meneja wa mkoa Kigoma Injinia Mathias Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Injinia Jones Mbike sambamba na kumzawadia fedha dereva wa Waziri huyo kwa utendaji uliotukuka.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa wilaya Kigoma,Esther Mahawe aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa watendaji hao wanastahili zawadi na heshima waliyopewa.
Mahawe alisema kuwa pamoja na changamoto zilizopo watendaji hao wamejitahidi kupambana katika kubuni na kusimamia miradi ya maji na kusogeza huduma kwa wananchi katika maeneo mengi ya mkoa huo.