Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI AWESO ATAKA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI UTOE MATOKEO

Eneo la chanzo cha maji Amani Beach manispaa ya Kigoma Ujiji. (Picha na Fadhili Abdallah)
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na miradi Wizara ya maji Abasi Muslim (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa maji Jumaa Aweso (wa tatu kulia) kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa chanzo cha maji Amani Beach ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma na vitongoji vyake.
(Picha na Fadhili Abdallah)
Waziri wa maji Jumaa Aweso (wa tatu kushoto) akipata maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa chanzo cha maji cha Amani Beach manispaa ya Kigoma Ujiji ambacho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi Bilioni 42 unaotekelezwa kwenye manispaa hiyo.


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAZIRI wa maji Jumaa Aweso amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya maji nchini lazima izingatie kuondoa kero na changamoto kubwa wanayopata wananchi ambao hawana huduma ya maji safi na salama kwa sasa.

Akizungumza wakati akitembelea eneo la mradi wa chanzo cha maji cha Amani Beach Manispaa ya Kigoma Ujiji waziri Aweso amewataka wakandarasi wa miradi ya maji nchini kuhakikisha miradi inamalizika kwa wakati kulingana na mikataba yao ili mipango ya serikali ya kupeleka huduma za maji safi na salama kwa wananchi iweze kutekelezeka.

Alisema kuwa haitoshi kueleza kuwa mradi umekamilika wakati huduma ya maji safi na salama haipatikani kwa wananchi hivyo wakandarasi na mamlaka za maji ambao ndiyo wasimamizi wa miradi hiyo wahakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi inakuwa kipaumbele cha utekelezaji wa miradi hiyo.

Waziri huyo wa maji alibainisha kuwa serikali ya awamu ya sita ya Raisi Samia Suluhu Hassan imepeleka fedha nyingi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji ili kutekeleza lengo la kumtua mama ndoo na maji yapatikane umbali mfupi kutoka kwenye makazi ya watu hivyo serikali haitakubali kuona miradi inayotekelezwa haitoi matokeo.

Akielezea utekelezaji wa ujenzi wa chanzo cha maji eneo la Amani Beach ambao ni sehemu ya mradi mkubwa wa maji kwenye manispaa ya Kigoma Ujiji wenye thamani ya shilingi bilioni 42 ametaka mradi huo ukamilike na kutimiza lengo la upatikanaji wa maji safi,salama na yanayotosheleza kwa wakazi wa mji huo na viunga vyake.

Awali akitoa taarifa kwa Waziri wa maji kuhusu utekelezaji wa mradi wa chanzo cha maji kwenye eneo la Amani Beach, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia miradi Wizara ya maji, Abasi Muslim alisema kuwa marekebisho ya chanzo hicho cha maji yanayotokana na usanifu upya uliofanywa utekelezaji wake umefikia asilimia 49 na muda wa kukamilisha mradi umekwisha.

Hata hivyo alisema kuwa mkandarasi ameomba muda wa ziada na serikali imekubali kumuongeza miezi mitatu kukamilisha mradi na kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo muda huo unatosha kukamilisha mradi kutokana na kazi ambazo zimeshafanyika na chanzo hicho kinaweza kuzalisha lita milioni 35 kwa siku.

Akizungumza katika ukaguzi wa mradi huo Mkuu wa wilaya Kigoma,Esther Mahawe alisema kuwa kazi kubwa imefanyika katika utekelezaji wa mradi huo wa maji kupeleka huduma kwa wananchi na kwamba changamoto ya kuungua kwa pampu za kusukuma maji kutokana na mawimbi makubwa ya ziwani ndiyo kumefanya malengo ya utoaji huduma kupungua.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa eneo ambalo linatumika kwa muda kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji safi na salama kwa wananchi imeweza kuondoa malalamiko na kero kubwa ya upatikanaji wa maji kwa wananchi na kwamba kukamilika kwa chanzo hicho kutawezesha Manispaa ya Kigoma Ujiji na viunga vyake kuwa na maji ya kutosha.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com