Mwanamke mmoja nchini Uganda amegonga vichwa vya habari kwa kufikia kile ambacho wanawake wengi wanaona ni maajabu yasiyo ya kawaida ikizingatiwa umri wake.
Mariam Nabatanzi ni mama mwenye umri wa miaka 41 ambaye ana watoto 44 anaowalea peke yake.
Aliyepewa jina la utani la Mama Uganda au Mama Afrika, Nabatanzi alifichua kuwa hataacha kuzaa.
Nabatanzi alisema watoto wake wote ni zao la uhusiano wake na mwanaume mmoja, ambaye alimtelekeza, kama ilivyoripotiwa na Afrimax English.
Alijifungua mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 13 tu baada ya kuozwa kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 57 nawazazi wake.
"Nilijifungua mara 15. Nilijifungua watoto wanne mara tano. Kwa mapacha ingekuwa mara sita, lakini kunao ambao waliaga dunia, hivyo ni mara tano pia," alisema.
Licha ya kulazimishwa kuolewa akiwa na umri wa miaka 12, Mariam alisema bado anaamini katika mapenzi ya kweli na kwamba ataendelea kujifungua pindi anapopata fursa.
"Ikiwa ningepata nafasi ya kukutana na mwanamume mzuri, ningefurahi kuzaa watoto zaidi kwa sababu kuzaa sio makosa. Kuzaa ni zawadi kutoka kwa Mungu," alisema.
"Nilikuwa nataka kujifungua watoto saba pekee," alisema.
Alisema alitaka kuwa na watoto watano na kuwataja majina ya ndugu zake waliofariki dunia, mmoja akiwa na jina lake na mwingine la mumewe.
"Mungu alifanikisha hili, na ndani ya mara mbili tu, tayari nilikuwa na watoto saba," Nabatanzi alifichua.
Alienda kwa madaktari kufunga uzazi wake na hata alitumia njia za kuzuia kupata uja uzito ili kuzuia kupata mimba, lakini yote yalikuwa bure.
“Kwa hiyo nikiwa na mwanaume ambaye ananielewa, nitakuwa na watoto zaidi,” Mariam alisema kwa furaha.