Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ANAYEDAIWA KUUA WATU SABA WA FAMILIA MOJA KIGOMA AKAMATWA..MAPENZI YAHUSISHWA


Kamishna wa operesheni na mafunzo jeshi la polisi Liberatus Sabas (kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (kulia) kuhusu kukamatwa kwa mtu mmoja akituhumiwa kuhusika na mauaji ya watu saba kwenye kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma. (Picha na Fadhili Abdallah)
Kamishna wa operesheni na mafunzo jeshi la polisi Liberatus Sabas (kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (kulia) kuhusu kukamatwa kwa mtu mmoja akituhumiwa kuhusika na mauaji ya watu saba kwenye kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma.


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WIVU wa mapenzi inaelezwa kuwa ndiyo chanzo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Peter Moris Mwandelema (33) kutekeleza tukio la kuua watu saba wa familia moja mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye kijiji cha Kiganza Kigoma Vijijini mkoani Kigoma ambapo Jeshi la polisi limemtia mbaroni mtu huyo.


Kamishna wa Operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi, Liberatus Sabas akitoa taarifa kwa  waandishi  wa habari mjini Kigoma jana alisema kuwa mtuhumiwa ambaye fundi ujenzi na mkazi wa eneo la Mlole mjini Kigoma alikamatwa jana mjini Kigoma.


Kamishna Sabas alisema kuwa kulingana na mahojiano na upelelezi uliofanyika polisi wamejiridhisha pasi na shaka kwamba mtuhumiwa huyo ndiye aliyehusika na tukio hilo la mauaji ya watu saba akiwa peke yake bila kushirikiana na mtu yeyote ambapo wananchi wametoa ushirikiano mkubwa wa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.


Akieleza chanzo cha tukio hilo Kamishna Sabas alisema kuwa mtuhumiwa Mwandelema alikuwa akimtuhumu Januari Mussa mmoja wa watu waliouawa katika tukio hilo kwamba alikuwa akitembea na mke wa mtuhumiwa ambaye kwa sasa jina lake limehifadhiwa.

Aidha Kamishna huyo wa operesheni na mafunzo alisema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya mauaji vinavyotokana na visa vya mapenzi jambo ambalo linatishia ustawi bora wa familia.

Akizungumzia hali hiyo Askofu wa Kanisa la EAGT kanda ya Magharibi, Omary Mlenda alisema kuwa watu kutokuwa na hofu ya Mungu ndiyo chanzo cha mauaji yanayotokea kwa binadamu kuuana.

Askofu Mlenda alisema kuwa haitoshi kuingia msikitini au kanisani kuonyesha kuwa mtu huyo ni muumini na ana hofu ya Mungu lakini matendo yake yanapaswa kuonyesha kwa vitendo ikiwemo kuwa na uvumilivu anapopatwa na jambo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com