Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja, akionyesha fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, (kushoto) ni Mke wake Zaituni Abdala, (kulia) ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Shinyanga mstaafu Charles Jishuli.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Hamis Mgeja ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mwaka 2007 hadi 2015, na kisha kuhamia CHADEMA na baadae kurudi tena CCM, amechukua fomu kuwania nafasi yake ya zamani ndani ya chama hicho.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 6, 2022 kwenye Ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kuchukua fomu hiyo ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa, amesema amejitathmini na kuona anafaa tena kuwa kiongozi.
Amesema yeye kama Mwanachama wa CCM ni haki yake ya kikatiba kugombea uongozi ndani ya Chama hicho, na baada ya kujitathmini ameamua tena kuchukua fomu na kugombea nafasi yake ya zamani ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
“Nimekuja kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuongoza nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kujitathmini na kuona naweza tena kuwa kiongozi, na nimetumia tu haki yangu ya kikatiba kama Mwanachama wa CCM,”amesema Mgeja.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa, amesema kwa sasa hawezi kutoa idadi ya wanachama ambao wamechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya Uenyekiti Mkoa hadi siku ya Mwisho ambayo ni Julai 10 ndipo atatoa idadi kamili.
Social Plugin