Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGODI WA MWIME WAJENGA SHULE MPYA


Muonekano wa majengo ya shule mpya kijiji cha Mwime.
Jengo la matundu 12, ya choo.
Muonekano wa majengo ya shule mpya kijiji cha Mwime.
Jengo la matundu 12, ya choo.
Meneja wa kikundi cha umoja wa wamiliki wa mashamba Kabela, Joseph Andrea Nalimi.


Na Paul Kayanda -  Kahama

MGODI wa Mwime uliopo Kata ya Zongomela Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga chini ya umoja wa kikundi cha wamiliki wa mashamba (KABELA) wamenunua ekari 5 kwa thamani ya Shilingi Milioni 10 na kuanzisha ujenzi wa shule mpya ya Msingi.

Kikundi hicho kimechukua uamuzi huo baada ya kuona shule ya Msingi Ilindi iliyopo mtaa wa Mwime kuwa na wingi wa watoto wanaosoma shuleni hapo ambao nni zaidi ya 2000 ukilinganisha asilimia kubwa umoja ya wanakikundi ni wazawa na eneo lao limebarikiwa na Mungu kuwa na Madini ya Dhahabu.

Meneja wa umoja wa wamiliki wa mashamba wa mgodi wa Mwime Joseph Nalimi aliyasema hayo juzi alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari waliotembelea Mgodi huo ili kujionea hali halisi ya maendeleo ya Mtaa wa Mwime kufuatia uwepo wa mgodi huo.


“Baada ya kukaa na serikali ya mtaa huu,tuliona kwenye suala la elimu shule yetu ya msingi imezidiwa sana na wanafunzi,tumejaribu kuwa tunajenga madarasa pale lakini hayawezi kutosha na tukabaini kuwa hata tukijenga madara 50 bado mwalimu mkuu atakuwa na mzigo mzito,” alisema Jeseph Nalimi meneja kikundi na kuongeza.

“Tuliona dawa ni kujenga shule mpya, kwa mana hiyo tukaomba mpango kazi ambapo mgodi tukalinunua eneo kwa gharama ya shilingi Milioni 10, tukalikabidhi kijiji na hati wanayo, wakampa taarifa mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ambaye akawapa milioni 120 za madarasa sita,” alisema.

Meneja huyo alisema kuwa mgodi unaunga mkono juhudi za mkurungenzi wa halmashauri kwa kujenga madarasa mawili ili kuongeza pamoja na ofisi mbili za walimu, na wakachimba karo na kujenga boma la choo matundu 12 wasichana 6 na wavulana 6 na kwamba tayari wamemkabidhi mkurugenzi kwa ajili ya umaliziaji.

Pamoja na mambo mengine meneja huyo alisema kuwa waliamua kujenga pia choo cha walimu matundu mawili na kukarabati ofisi ya kijiji kwa kuiezua paa na kuianza kuijenga upya mpaka rangi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Ilindi Dogo Mheziwa alipongeza Mgodi huo kupitia kikundi cha umoja wa wamiliki wa mashamba kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi wake huku akisema kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya manispaa ya Kahama Anderson Msumba ameunga mkono juhudi za mgodi huo kwa kuchangia shilingi Milioni 120 za umaliziaji katika shule mpya ya msingi Mwime.

Kufuatia hali hiyo Mheziwa alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuupandisha hadhi mtaa wa Ilindi kuwa Kata ya Mwime badala ya Kata ya Zongomela kutokana na maendeleo kuwa ya kasi kwenye eneo hilo kufuatia uwepo wa mgodi.

“Sensa ya watu na makazi kwa mtaa wa Ilindi na Mwime itasaidia kujua idadi ya watu na kupata Kata, kutoka mtaa wa Ilindi kwenda makao makuu ya Kata Zongomela ni lazima uvuke kata jirani ya Mhungula ndipo ufike kata ya Zongomela naomba serikali iliangalie hilo,” alisema Mheziwa.

Alisema kuwa wananchi wanapata adha ya kupata huduma ya kiofisi huko Zongomela kwani wanatembea umbali mrefu kilomita tatu ndipo unafika makao makuu, kwa wazee wajawazito ni changamoto lakini iwapo serikali itasikia kilio hicho itakuwa imesogeza huduma karibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com