Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Sophia Mjema akizungumza wakati wa kuwaaga wanafunzi kwenda kwenye mashindano ya UMITASHUMTA
Afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Bi. Dafroza Ndalichako wakati akizungumza
Wanafunzi wanaokwenda Mkoa wa Tabora kuuwakilisha Mkoa wa Shinyanga kwenye mashindano ya UMITASHUMTA
*
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amewataka wanafunzi wote waliopata nafasi ya kuchaguliwa kuwakilisha mkoa katika mashindano ya kitaifa ya michezo kwa wanafunzi kote nchini kuhakikisha wanasimamia nidhamu na kufanya vizuri ili wapate kurudi na kombe wakati wa kuhitimishwa kwa mashindano hayo.
Rc Mjema amewaasa wanafunzi hao wapatao 120 na viongozi 16 ambao wamekuwa pamoja toka kuanza kwa Maandalizi ya mashindano hayo yaliyoanza tarehe 18.07.2022 na yatahitimishwa tarehe 21.08.2022 kitaifa Mkoa wa Tabora.
Amewasihi wanafunzi hao waliopata nafasi ya kuwakilisha mkoa wakitokea katika kila wilaya na Halmashauri zinazounganisha Mkoa wa Shinyanga kudumisha nidhamu, kuwa na umoja pamoja na kuhakikisha wanasikiliza maelekezo ya waalimu wao ili waweze kuleta ushidi kwa mkoa wakati watakaporejea
Amesema serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha michezo inaboreshwa na inawekewa mkazo kwani upo umuhimu mkubwa wa kuhakikisha wanafunzi pamoja na masomo wanayopata lakini michezo inawasaidia katika kujiweka sawa kimwili na kuondokana na mawazo potovu ambayo yanaweza kumfanya mwanafunzi akashindwa kuweka akili yake katika masomo na kujituma.
"Ninawatuma muende mkatuwakilishe vizuri huko Tabora mnakokwenda na mkasikilize kwa umakini mafunzo na maelekezo mtakayopewa kwa ufasaha mimi nataka mkirudi mlete kombe hapa pamoja na kombe la nidhamu nawaomba sana msiende kuniwakilisha kwa aibu huko muendako na Mungu akawasimamieni vyema mnapoenda kukutana na wanafunzi wenzenu kutoka Mikoa tofauti tofauti", amesema Mjema.
Pia Mkuu wa Mkoa akiwa pamoja na Kamati ya ulinzi ya Mkoa kwa pamoja wamegawa vifaa na zana zote zitakazowasaidia wanafunzi hao katika Mashindano hayo.
Kwa upande wake Afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Bi. Dafroza Ndalichako amesema Mkoa umetumia vigezo vyote katika kuhakikisha inawapata wanafunzi ambao watauwakilisha Mkoa katika mashindano hayo huku wakisaidiana na walimu wao wa michezo katika kuhakikisha wanaleta ushindi kwa Mkoa mzima
Akitaja michezo ambayo itakwenda kushindaniwa ni pamoja na Mchezo wa Mpira wa Mguu( football) Mpira wa net ( Netball) Mpira wa Volleyball, michezo ya Sanaa ikiwa ni pamoja na michezo maalumu kwa ajili ya makundi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kama ya wasioona, wasiosikia na wenye ulemavu