Mhasibu wa Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI), Joseph Kulwa akielezea namna wanavyosindika zao la mkonge. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Usindikaji zao la mkonge ukiendelea katika Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI)
Mhasibu wa Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI), Joseph Kulwa akionesha mkonge uliosindikwa tayari kusafirishwa kwenda kwa wanunuzi
Mwenyekiti wa Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI), akielezea kuhusu usindikaji wa mkonge.
Mbunifu wa mitambo ya kuchakata zao la mkonge Daud Magili Magolyo mkazi wa Kishapu akielezea kuhusu mtambo mpya wa kisasa zaidi wa tatu kubuniwa duniani aliotengeneza kwa ajili ya kutumika kusindika mkonge.
Mbunifu wa mitambo ya kuchakata zao la mkonge Daud Magili Magolyo mkazi wa Kishapu akionesha namna mtambo mpya wa kisasa unavyofanya kazi ya kusindika mkonge.
Msaidizi wa Mbunifu wa mitambo ya kuchakata zao la mkonge Daud Magili Magolyo mkazi wa Kishapu akionesha mkonge uliosindikwa kwenye mtambo mpya wa kisasa wa kusindika mkonge.
Muonekano wa bango katika kitalu cha miche ya mkonge Kishapu
Muonekano wa miche katika kitalu cha miche ya mkonge Kishapu
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wananchi katika Halmashauri ya Kishapu wamehamasika kulima zao la Mkonge huku changamoto kubwa sasa ikiwa ni uhaba wa miche ya mbegu licha ya kwamba halmashauri hiyo imeanzisha kitalu chenye ukubwa wa ekari 20 kinachokadiriwa kuwa na miche 640,000.
Hamasa hiyo imetokana na maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipokutana na wadau wa mkonge mkoani Tanga mwaka 2021 ambapo alihamasisha Mikoa yenye ukame kama Kishapu kuona zao la Mkonge kama fursa ya zao la biashara badala ya kuwa zao mbadala jambo ambalo amekuwa akilihamasisha kila mara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa serikali kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo mkonge.
Kufuatia agizo hilo, wananchi wa Kishapu wamehamasika kulima zao hilo na sasa mahitaji yao ni miche milioni 13 juu ya kiwango cha miche iliyopo sasa 640,000 katika kitalu cha miche ya mkonge kilichoanzishwa na Halmashauri ya Kishapu.
Akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo waliotembelea wadau wa kilimo wilayani Kishapu, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika (Afisa Ugani) wilaya ya Kishapu, George Kessy amesema wakulima wa Kishapu wamehamasika kulima zao la mkonge na kinachohitajika sasa ni miche.
“Tumelima kitalu cha miche ya mkonge chenye ekari 20 kwa ajili ya kuzalisha miche tutakayoisambaza kwa wakulima, tayari wakulima wamejitokeza kwa wingi wakihitaji miche zaidi ya milioni 13 na mwezi Oktoba miche iliyopo tutaanza kuisambaza kwa wananchi ”,amesema Kessy.
“Tayari tuna Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI) ambao walima na kusindika mkonge na tunaye mbunifu wa mitambo ya kuchakata zao la mkonge Daud Magili Magolyo ambaye serikali imekuwa bega kwa bega naye katika kuhakikisha teknolojia hiyo inakuwa bora zaidi na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya teknolojia na viwanda wamekuwa wakimtembelea na kumpa ushirikiano na sasa amehama kutoka kwenye mashine za kwanza za kawaida na ametengeneza mtambo mpya wa kisasa zaidi wa tatu kubuniwa duniani”,ameeleza afisa ugani huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson amesema wananchi wamehamasika kulima zao la mkonge na mahitaji ya miche ni makubwa hivyo ili kupata miche mingi ya mkonge wanaendelea kuhamasisha wananchi kuanzisha vitalu vyao binafsi.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude amesema hivi sasa kuna mabadiliko makubwa kwani wananchi wameanza kuchangamkia kilimo cha mkonge zao ambalo linastahili ukame kulingana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mhasibu wa Shirikisho la wakulima na wasindikaji Mkonge Kishapu (SHIWAMKI), Joseph Kulwa amewashauri wananchi wakiwemo vijana kuchangamkia fursa ya zao la mkonge kwani halina msimu na linavumilia ukame na soko lake ni kubwa ili kujikwamua kiuchumi.
“Soko la mkonge sasa ni kubwa na kupitia SHIWAMKI tumefanikiwa kuuza tani 240,000 na sasa tunauza kilo moja shilingi 2500”,amesema.
Social Plugin