Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT.GWAMAKA AFANYA ZIARA KUTEMBELEA BANDARI YA MTWARA KUKAGUA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI WA MAKAA YA MAWE

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ametoa Rai kwa wawekezaji wa Makaa ya Mawe kote Nchini kuhakikisha wanazingatia utekelezaji wa Sheria ya utunzaji wa mazingira ya Mwaka 2004 hususani ya ufanyaji wa tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya uwekezaji.

Rai hiyo imetolewa leo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi Bandari ya Mtwara kukagua miundombinu ya kusafirisha Makaa ya Mawe nje ya Nchi inayofanywa na wawekezaji wa Makaa ya Mawe.

Amesema wawekezaji hao wengi wao wameingia mikataba ya kufanya biashara hiyo bila kupata kibali cha tathmini ya athari kwa mazingira hali inayoweza kuhatarisha maisha ya wakazi wa eneo husika, mimea na viumbe hai.

" Unapofanya tathmini ya athari kwa mazingira unakuwa katika nafasi nzuri ya kulinda na kuyahifadhi mazingira, Lakini pia unaleta usawa kwa wafanyabiashara, lakini pia inatunza mazingira na kumpa muwekezaji uhakika wa kufanya biashara bila bugudha yeyote" Amesema Dkt. Gwamaka.

Kadhalika Mkurugenzi Gwamaka amemtaka muwekezaji kujenga ghala la kuhifadhia Makaa hayo ya Mawe kwani yasipohifadhiwa vizuri yanaweza kuleta athari kwa mazingira na afya kwa ujumla hasa ikizingatiwa Makaa hayo yanayo madini ambayo si rafiki kwa binadamu na mazingira.

Naye Meneja Kanda ya Kusini Mtwara inayohusisha Mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi Mhandisi Boniphace Guni alipozungumza amesema atahakikisha maelekezo yote hayo yanatekelezwa ikiwa ni pamoja na kusimamia suala zima la utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inayosisitiza ufanyaji wa tathmini ya mazingira kabla ya uwekezaji.

Mkurugenzi Gwamaka katika ziara yake hiyo ametembelea maeneo matatu yanayohifadhi Makaa ya Mawe tayari kusafirishwa nje ya Nchi ambayo ni eneo la bandari ya Mtwara iliyopo Kampuni ya Ruvuma Coal limited, eneo la STAMIKO pamoja na eneo lililoko nje ya bandari ambaye muwekezaji wake ni kampuni ya SEBDO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com