Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) Said Mankiligo akizungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga (SHIREFA) Said Mankiligo akizungumza na waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano (PRESS CONFERENCE) na Chama Cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga (SHIREFA).
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
CHAMA cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga (SHIREFA), kimewaita viongozi wa Timu ya Stendi United na Mwadui Fc, wakae mezani na kupanga mikakati ya kuzipandisha timu hizo kushiriki kucheza ligi daraja la kwanza na hatimaye ligi kuu.
Mwenyekiti wa SHIREFA mkoani Shinyanga Said Mankiligo, amebainisha hayo leo Julai 9, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Chama hicho cha Mpira wa Miguu.
Amesema Mkoa wa Shinyanga hauna Timu ambayo inashiriki kucheza ligi kuu tofauti na misimu iliyopita, ambapo Timu hizo mbili Stendi United na Mwadui Fc zilishiriki kucheza ligi kuu, lakini zikatolewa na zikashuka daraja, na sasa Timu hizo zote mbili zipo daraja la Pili.
“Chama cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga tunawaomba viongozi wa Timu ya Stendi United na Mwadui FC tukutane nao na kupanga mikakati ya pamoja, ili kuzipandisha Timu hizi kutoka daraja la Pili hadi la kwanza, na baadae zipande hadi ligi kuu,”anasema Mankiligo.
Aidha, ameziomba Timu hizo pia zifanye usajili wa wachezaji katika kipindi hiki cha usajili, ili wapate wachezaji wazuri ambao watazipatia matokeo na kutimiza malengo yao.
Katika hatua nyingine, amewaagiza viongozi wa Soka ngazi za wilaya, ambao bado hawajaanzisha mashindano ya ligi katika wilaya zao kuhakikisha, wanakamilisha maandalizi hayo ndani ya mwezi huu ili ligi zianze mara moja.
Pia, amesema mwakani wanatarajia kukaribisha mashindano ya Ndondo Cup mkoani humo ili kuibua vipaji vya vijana.