*******
NA EMMANUEL MBATILO
Kwa mara nyingine tena Yanga inabeba ubingwa msimu huu mara baada ya kufanikiwa kunyakua kombe la Azam Sports Federation Cup kwa kuwachapa Coastal Union kwa mikwaju ya penati 4-1.
Fainali hii imekuwa ni yakuvutia hasa licha ya Coastal Union kucheza kandanda safi kwa vipindi vyote kwani waliweza kupachika mabao mazuri ambayo hayakusaidia kabisa kuwatawaza mabingwa.
Abdul Sopu ndiye tuseme ni mchezaji ambaye amekuwa kivutio kwa yeyote ambaye ameangalia mpira huu mpaka mwisho kwani ameweza kupachika bao tatu peke yake kwenye mchezo huo.
Kwenye mchezo huo ambao ulipigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid Jijin Arusha, Coastal Union walianza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao hatari Abdul Sopu dakika ya 11 ya mchezo na kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza.
Kipindi cha pili Yanga Sc ilisawazisha bao kupitia kwa Feisal Salumu na baadae Heritie Makambo kupachika bao la pili dakika ya 81 kabla ya Abdul Sopu kusawazisha kwa upande wa Coastal Unions dakika za lala salama.
Baada ya dakika 90 kumalizika ziliongezwa dakika 30 kutafuta mshindi wa fainali hiyo ambapo Sopu tena aliweza kuwalaza Yanga sc kwa bao safi kabisa akimtoka beki wa Yanga Kibwana Shomari lakini baadae Nkane aliweza kusawazisha bao na kwenda matuta.