AJALI YA GARI NA MKOKOTENI YAUA WATU SABA DODOMA

 WATU saba wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Landcruiser yenye namba za usajili STL 9534 mali ya Idara ya maji mkoa wa Katavi, kugonga kwa nyuma mkokoteni uliokuwa unavutwa na ng’ombe katika Kijiji cha Lugala- Kata ya Manzase wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.



Ajali hiyo imetokea leo tarehe 3 Julai, 2022 saa 11 alfajiri wakati gari hiyo ikitokea Dodoma kuelekea Mtera kugonga mkokoteni huo uliokuwa ukikokotwa na ng’ombe wawili huku ukiwa umepakia abiria 12.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amethibitisha kutokea ajali hiyo na kubainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa gari hiyo.

Amesema mbali na watu hao saba, pia ng’ombe wawili waliokuwa wakikokota mkokoteni huo, nao pia wamefariki kutokana na ajali hiyo.


Amesema gari hiyo ilikuwa inaendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Paschal Sitta mkazi wa Katavi, alikuwa akiendesha gari hiyo kwa mwendokasi ambao ulimsababisha kushindwa kung’amua iwepo wa mkokoteni huo mbele yake kwa haraka.

“Kwa sababu muda huo wa alfajiri hilo eneo huwa linakuwa na ukungu kidogo, sasa kwa kuwa dereva alikuwa speed kwa uelekeo sawasawa na huo mkokoteni kama wanaelekea Iringa, alipoukaribia mkokoteni huo na ukizingatia huaukuwa na alama zozote nyuma, basi akaugonga, ukapinduka, watu saba wakafariki papo hapo, na ng’ombe wawili,” amesema.

Amesema majeruhi watano wa ajali hiyo wamewahishwa katika hospitali ya General mkoani Dodoma kwa ajili ya matibabu.



Source: Mwanahalisi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post