WATETEZI HAKI ZA BINADAMU,CCM WALAANI MAUAJI YA WATU SABA KIGOMA


Mratibu wa kanda ya Magharibi wa mtandao wa haki za binadamu nchini (THRDC) Alex Luoga akizungumza na waandishi wa Habari akitoa tamko la kulaani mauaji ya watu saba waliouawa kijiji cha Kiganza wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma. Picha na Fadhili Abdallah)


Katibu wa CCM mkoa Kigoma Mobutu Malima akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiganza alipofika kijijini hapo kutoa pole kwa tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita

Na Fadhili Abdallah,Kigoma


MASHIRIKA mashirika 25 ya watetezi wa haki za binadamu kanda ya magharibi inayojumuisha mikoa ya Kigoma,Tabora na Katavi wamelaani tukio la mauaji ya watu saba yaliyotokea kwenye kijiji cha Kiganza wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.

Mratibu wa kanda ya Magharibi wa Mtandao wa haki za binadamu nchini (THRDC), Alex Luoga akisoma tamko kwa niaba ya mashirika hayo alisema kuwa ni tukio la kusikitisha na kuhuzunisha ambalo linapaswa kulaani kwa nguvu zote.

Luoga alisema kuwa vitendo vya mauaji ya kinyama kama hayo yanapaswa yapigwe vita kwa namna yeyote ambapo wametoa wito kwa serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kuwasaka na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kufanya mauaji hayo.

Katika tamko lao watetezi hao wa haki za binadamu wameliomba jeshi la polisi kutoa tamko la kuwataka waliofanya mauaji hayo kujisalimisha sambamba na kutoa zawadi kwa watu wema watakaotoa taarifa za wahusika.

Luoga alisema katika tamko hilo kuwa wanalipongeza jeshi la polisi kwa kuchukua hatua za haraka kuunda kikosi maalum cha kushughulikia tukio hilo chini ya Kamishna wa Operesheni na mafunzo,Liberatus Sabas na kutaka uchunguzi ufanyike kwa makini na itendeke kwa wahusika.

Aidha watetezi hao walisema kuwa ni kinyume cha hake za binadamu kwa wananchi kuchukua hatua mkononi kuondoa uhai wa watu wengine na kwamba inapotokea tatizo wapeleke kwenye mamlaka zinazohusika liweze kushughulikiwa kwa hatua za kisheria.

Pamoja na hivyo watetezi hao wametoa pole kwa familia ya watu hao na serikali kwa hatua walizochukua kushughulikia tatizo hilo na hasa kuhakikisha tukio hilo halizui taharuki na woga kwa wananchi.

Katika hatua nyingine CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimelaani mauaji ya watu saba wa familia moja yaliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili wiki iliyopita katika kijiji cha Kiganza Halamshauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma.

Katibu wa CCM mkoa Kigoma,Mobutu Malima akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alipofika kutoa pole kwa wafiwa amesema kuwa haikubaliki kwa namna yeyote kuona binadamu wanachinjana kama kuku na kutaka hatua za haraka za kuwatafuta watuhumiwa zipewe nguvu ya kutosha.

Katibu huyo wa CCM mkoa Kigoma alisema kuwa siyo utaratibu wa mila na tamaduni za watanzania kufanyiana matukio ya kinyama kama hilo ambalo ni kinyume na masuala ya ubinadamu na kwamba CCM ina laani kwa nguvu mauaji hayo.

“Ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tukio hili na nina mashaka sana kama hakuna mkono wa raia kutoka nje ya nchi ambao wamehusika kwa namna yeyote ikiwemo kukodiwa kufanya mauaji hayo,”Alisema Malima.

Kutokanana hilo alisema kuwa wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi yao ni vizuri wananchi wakatoa ushirikiano wa kutosha kuwafichua wahusika ili hake iweze kutendeka kwa kuchukuliwa hatua kwa unyama walioufanya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post