Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHAKA ATEMBELEA VYOMBO VYA HABARI ZANZIBAR


Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka leo amefanya ziara katika vyombo mbalimbali vya habari kisiwani Unguja.

Shaka ambaye ameanza ziara ya siku nne visiwani Zanzibar kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, alitembelea Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Kituo Cha Redio Cha Bahari FM na Zenji FM.

Kote huko alipata nafasi ya kufafanua masuala mbalimbali. Kuhusu suala la utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 -2025, vipaumbele vya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, maridhiano na taathimini ya awali ya hali ya uchanguzi ndani ya Chama, Shaka alitoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, alisema utulivu uliyopo Zanzibar kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kumetoa nafasi kwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzidisha kasi ya maendeleo Zanzibar

Akizungumzia suala la Sensa ya Watu na Makazi, Shaka amesema ni muhimu sana katika mipango ya maendeleo.

“Juzi Jumamosi umoja wa Mataifa ulitoa ripoti ya idadi ya watu duniani kwamba Tanzania ni kati ya nchi nane duniani zitakazochangia nusu ya idadi ya watu billioni 9.7 ifikapo mwaka 2050.. na kwamba hii itazuia kazi ya kuondoa umasikini...sasa sensa yetu itatoa nafasi kwa wataalamu waje watuambie kama tupunguze kuzaana au la...na kubwa zaidi serikali itajua idadi ya watu ili ipange mipango ya maendeleo vizuri ". alisema Shaka

Shaka anaendelea na ziara yake kesho tarehe 14 Julai, 2022 ambapo ataelekea kisiwani Pemba.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com