Polisi eneo la Kaimosi katika Kaunti ya Nandi wameanzisha msako wa kumnasa mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 17 kwa tuhuma za kumuua binamu yake. Mvulana huyo alimuua binamu yake kwa kumdunga kwa mshale.
Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), mshukiwa alimuua Josephat Kibet mwenye umri wa miaka 31 kufuatia mzozo wa kuchaji simu.
Taarifa ya DCI inasema kuwa mzozo kati ya wawili hao ulizuka jioni ya Jumapili, Julai 10, na kinda huyo kumshambulia binamu yake.
“Polisi eneo la Kaimosi, Kaunti ya Nandi wanamtafuta mshukiwa wa miaka 17 ambaye alimuua binamu yake jioni ya Jumapili kufuatia mzozo wa kuchaji simu. Kufikia sasa uchunguzi unaonyesha kuwa wawili hao walikuwa wakizozana kuhusu ni nani wa kuchaji simu yake wa kwanza,” DCI ilisema kupitia kwa taarifa.
Mshukiwa anaripotiwa kuchomoa mshale na kumdunga binamu yake kabla ya kukimbilia mafichoni.
“Mvulana huyo alikimbia mshale na kumdunga mwendazake upande wa kushoto wa kifua kabla ya kutoroka,” DCI ilisema.
Josphat KIbet alikimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Kapsabet lakini akawa ameaga dunia hata kabla ya kufikishwa hospitalini.
“Josphat Kibet alithibitishwa kuaga dunia alipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kapsabet kufuatia majeraha na mshale kutoka kwa kinda huyo,” taarifa ya DCI inasema.
Social Plugin