Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB NA IFC KUONGEZA UPATIKANAJI WA MITAJI KWA WAJASIRIAMALI NCHINI TANZANIA NA BURUNDI


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta (kulia) wakibadilishana mikataba ya makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam.

======== ======= ========
Benki ya CRDB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) leo wameingia mkataba wa uwezeshaji utakaongeza upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali wadogo na wakati nchini Tanzania na Burundi, na kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili kutokana na athari za janga la UVIKO-19. Hafla hiyo ilifanyika katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi waaandamizi wa taasisi hizo.


Chini ya ushirikiano huo, IFC inatoa mkopo wa dola milioni 100 kwa Benki ya CRDB Tanzania, nusu ya fedha hizo zitakuwa kwa shilingi ya kitanzania, na mkopo wa dola milioni 5 kwa Benki ya CRDB Burundi kusaidia mikopo kwa wafanyabiashara wadogo katika nchi zote mbili, hasa kwa wafanyabiashara wanaomilikiwa na wanawake.


Katika mkataba huo, asilimia 25 ya mkopo unaoelekezwa nchini Tanzania utatolewa kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake. Imebainishwa kuwa fedha hizo zitaongeza upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, ambayo imekuwa adimu kupatikana tangu kuzuka kwa janga la COVID-19.

Mikopo hiyo ni sehemu ya mpango wa IFC wa uwezeshaji wa tabaka la chini katika uchumi, ambao unalenga kusaidia taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabisahara wadogo ambao wameathiriwa zaidi na janga la UVIKO-19. Ufadhili wa IFC pia unasaidiwa na Dirisha la Sekta ya Binafsi la Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa.

Wajasiriamali ni kundi muhimu kwa uchumi wa Tanzania na Burundi. Nchini Tanzania, wastani wa biashara ndogo ndogo na za kati ni milioni 3.2, huchangia asilimia 27 ya Pato la Taifa, na kuajiri zaidi ya watu milioni 5. Hata hivyo, takriban asilimia 81 ya biashara hizi hazina uwezo wa kupata fedha. Biashara nchini Burundi pia zinachangamoto kubwa katika kupata fedha.


"Fedha hizi zimekuja wakati muafaka na zitaongeza uwezo wetu wa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati huku tukisaidia kuongeza usawa wa kijinsia katika mnyororo wa thamani. Benki ya CRDB tunaamini kuwa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ni msingi wa maendeleo. Wanawake wameathirika kwa kiasi kikubwa sana janga la UVIKO-19, ambalo limepelekea changamoto nyingi za kiuchumina kuathiri moja kwa moja maisha ya familia na jamii zao,” alisema Abdulmajid Nsekela Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB wakati wa hafla ya utiaji sahihi.


Nsekela aliongezea kuwa ufadhili wa IFC utasaidia maendeleo ya sekta mbalimbali za maendeleo nchini, ikiwamo biashara, kilimo, afya, elimu, makazi, na miundombinu. Maeneo mengine ni pamoja na miradi inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, wajasiriamali, pamoja na biashara zinazomilikiwa na wanawake kama ambavyo imesisitizwa katika mkataba huo wa ushirikiano baina ya Benki ya CRDB na IFC.


“Ushirikiano kati ya IFC na Benki ya CRDB utasaidia ukuaji wa sekta ya ujasiriamali katika nchi hizi ambapo mchango wao katika ajira na shughuli za kiuchumi ni mkubwa. Ushirikiano huu pia unajumuisha jitihada maalum katika kusaidia biashara zinazomilikiwa na wanawake na kuendeleza ushirikishwaji wa kijinsia, ikiwa ni sehemu muhimu ya mkakati wa IFC nchini Tanzania na Afrika," alibainisha Sérgio Pimenta, Makamu wa Rais wa IFC Afrika.

IFC ina uhusiano wa muda mrefu na Benki ya CRDB. Mkataba huo wa makubaliano wa uwezeshaji kibiashara uliowekwa sahihi leo ni wa tano baina ya taaisi hizo, na ni sehemu ya kazi inayokua ya IFC nchini Tanzania kusaidia ukuaji wa biashara ndogo ndogo na kukuza uwezeshaji kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta (kulia) wakitia saini mkataba wa makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akizungumza katika hafla fupi ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam. kulia ni Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com