Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANASIASA WAKONGWE LEMBELI NA MGEJA WALIVYOONGEZA JOTO LA UCHAGUZI CCM SHINYANGA


Khamis Mgeja na James Lembeli (kulia) - Picha kutoka Maktaba yetu
James Lembeli akiwa ameshika fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja, akionyesha fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga

Na Paul Kayanda - Kahama

VUGU vugu la Uchaguzi ndani ya CCM Mkoa wa Shinyanga linazidi kushika kasi kufuatia wanasiasa wakongwe katika Mkoa wa Shinyanga na hapa nchini Khamis Mgeja pamoja na James Lembeli aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Kahama baada ya wawili hao kuchukua fomu ili kugombea nyadhifa katika chama.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa kuchukua fomu hiyo,Lembeli alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kujipima na kujitathmini na kujiona kuwa nafasi hiyo anaiweza kwa sababu ana uzoefu ndani ya Chama, na pia ni kiongozi mzoefu ndani na nje ya nchi na anaweza kuongoza vizuri Chama.

Lembeli ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira (2010-2015),amesema Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, kinahitaji viongozi thabiti, makini na hawana makando kando, sifa ambazo anazo na kuamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti CCM katika mkoa wa Shinyanga.

“Nmejitathmini nikaona nije nichukue fomu ili nigombee nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwa sababu sifa zote zote ninazo, hasa katika zama hizi ambapo kuna changamoto nyingi za hapa na pale na chama kinahitaji mtu jasiri mwenye uwezo wa kusukuma mbele maendeleo ya chama,” amesema James Lembeli kada wa CCM Kahama.

Makada wa CCM wameendelea kuchukua fomu za kuwania uongozi ambapo Julai 6 mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja (2007-2015) kisha akahamia CHADEMA na kurudi tena CCM, alianza kuchukua fomu ya kugombea tena nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa huo kabla ya Lembeli, uchaguzi ambao utafanyika mwaka huu 2022.

Huku Mabala Mlolwa naye akionyesha nia ya kuendelea kutetea kiti chake ambacho mpaka sasa anawaongoza wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza na Tanzania Daima jana mjini Kahama Mgeja amepongeza chama cha Mapinduzi (CCM) kufungua milango ambapo kila mwanachama anahaki ya kutimiza wajibu wake kikatiba kuomba ridhaa ya kugombea au kuchaguliwa.

“Hii ni kuendeleza demokrasia katika chama na inaendelea kudhilisha ukomavu wa kisiasa ndani ya chama chetu,” alisema Mgeja huku akisema mambo mengine ni kusubili uamuzi wa chama chenyewe.

Mgeja amewahi kutumikia nyadhifa mbalimbali katika chama na serikali ambapo amewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa,Mwenyekiti wa umoja wa Vijana UVCCM Mkoa wa shinyanga, Mjumbee wa baraza kuu la vijana Taifa na mjumbe wa kamati ya utekelezaji Taifa.

Vile vile Mgeja amewahi kuwa Diwani wa Kata ya kilago na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama,Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu Mkoa wa shinyanga, (SHIREFA), Mjumbe wa mkutano mkuu Taifa chama cha mpira Tanzania TFF, Mjumbe na makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) na Mjumbe wa kamati tendaji ya Red Cross Mkoa wa Shinyanga.

Na mpaka sasa ni mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation taasisi inayojishughulisha na masuala ya haki Demokrasia na utawala bora, Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo Mkoa wa Shinyanga waislamu (Bakwata) nan i mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Kahama United Sports Academy.

Kwa sasa anayetetea kiti chake Mabala Mlolwa ambaye pia ni diwani wa Kata ya Chona Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama ni sehemu ya wagombea kiti hicho.

Hata hivyo uchukuaji wa fomu ngazi ya Wilaya katika chama na jumuiya zake ulihitimisha juzi tarehe 13, mwaka huu kote nchini, wakati huo uchukuaji wa fomu na urejeshaji wa fomu hizo ngazi ya Mkoa na Taifa chama pamoja na jumuiya zake mwisho ni tarehe 10 Augosti mwaka huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com