Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Masijala Kuu, imekubali maombi ya wabunge 19 wa Viti Maalum wakiongozwa na Halima Mdee, kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama pamoja na kuiomba mahakama ifanye mapitio ya kimahakama ya mchakato uliotumika kuwavua uanachama.
Uamuzi huo umetolewa leo Julai 8, 2022, na Jaji Mustafa Ismail, baada ya kusikiliza maombi hayo yaliyokuwa yamefunguliwa na akina Mdee dhidi ya CHADEMA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Akisoma Uamuzi huo, Jaji Ismail amewataka kina Mdee wafungue kesi hiyo ndani ya siku 14 kuanzia leo.
Katika maombi hayo, Mdee na wenzake 18 waliiomba mahakama ifanye mapitio ya kimahakama dhidi ya mchakato ambao CHADEMA ulitumia kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali kwani haukufuata sheria kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kusikilizwa na kugubikwa na upendeleo.
Hata hivyo, Chadema kupitia mawakili wake, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, waliiomba mahakama ikatae ombi la kina Mdee kwa kuwa hoja zao hazina mashiko wakidai walipewa nafasi ya kusikilizwa.
Mbali na Mdee, wabunge wengine ni Jesca Kishoa, Ester bulaya, Esther Matiko, Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Angesta Lambart, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.
Mdee na wenzake walituhumiwa kwa makosa ya kusaliti msimamo wa CHADEMA wa kutopeleka wawakilishi wake bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kwa madai kwamba haukuwa huru na wa haki.
Mdee na wenzake walivuliwa rasmi uanachama wa Chadema Mei 12 mwaka huu na baraza la wadhamini la chama hicho.
Chanzo - Michuzi blog