Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TCRA : VICHWA VYA HABARI KWENYE BLOGS , ONLINE TV VIENDANE NA KILICHOMO NDANI.... 'IMEISHA HIYO'

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii ikiwemo Blogs na Youtube (Bloggers & Youtubers) kufanya kazi kwa weledi wakizingatia Sheria na Kanuni zinazowaongoza.

Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo ametoa rai hiyo Julai 06, 2022 jijini Mwanza, wakati akifungua kikao kazi baina ya TCRA na waandishi wa habari wa vyombo habari mtandaoni kilicholenga kujengeana uelewa kuhusu mabadiliko madogo ya Kanuni za maudhui mtandaoni.

Mhandisi Mihayo amesema baada ya sekta ya habari mtandaoni kukua hapa nchini, zimeibuka changamoto mbalimbali ikiwemo upotoshaji unaofanywa na baadhi ya runinga za mtandaoni ambapo kichwa cha habari kinakuwa hakina mahusiano na maudhui yaliyo ndani ya habari.

“Unakuta kichwa cha habari kimeandikwa ‘Imeisha Hiyo’ ukiingia ndani unakuta mwanzo hadi mwisho mtangazaji anasema na neno ‘Subcribe, bonyeza kengele’ kwa habari zaidi, sasa hiyo kwa wataalamu wenye leseni kutoka TCRA sitegemei muwe na kitu kama hicho” amesema Mhandisi Mihayo.

Pia Mhandisi Mihayo amesema kuna baadhi ya makosa yamekuwa yanafanywa na vyombo vya habari kwa kujumuisha taasisi nzima pale mtumishi mmoja anapokuwa ametenda kosa lisilo la kimaadili jambo ambalo amesema si weledi.

“Mfano labda mimi ni mlevi na nimekamatwa huko mtaani nazurura, badala ya kusema Mhandisi Mihayo nimekamatwa, mnaandika TCRA yaendekeza ulevi, hiyo si sawa, mnatakiwa kudili na mimi bila kuingiza TCRA” amesisitiza Mhandisi Mihayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza, Edwin Soko akiwasilisha mada kuhusu usalama wa waandishi wa habari mtandaoni, amesema wanapaswa kuwa makini kwa kuimarisha ulinzi wa vifaa vyao mtandaoni ili kuepuka kudukuliwa kwani hiyo ni changamoto kubwa kwa sasa.

“Kuna mambo mbalimbali yanayoashiria vitisho vya kimtandao ambayo mnatakiwa kuwa nayo makini ikiwemo kutoshawishiwa kubonyeza ‘links’ zinazoshawishi kwamba umeshinda zawadi (phishing). Mwaka 2013/15 Facebook na Google walilipa dola milioni 100 kwa watu wasiowahusika baada ya kudukuliwa kutokana na kubonyeza ‘links za aina hiyo” amesema Soko huku akihimiza watumiaji wa mitandao ya kijamii kukinga vifaa vyao kwa kuweka nywila (password) na programu za kupambana na wavamizi mtandaoni (Malware Virus).

Akiwasilisha mada kuhusu maadili ya uandishi wa habari, Mwenyekiti Mstaafu wa MPC Deus Bugaywa amesema changamoto iliyopo kwenye vyombo vya mtandaoni ni kutopitia kwenye dawati la uhariri wa zaidi ya mtu mmoja na hivyo kuwa na makosa mengi ya kimaadili ambapo wengi wa watoa maudhui wamekuwa wakitaka kuwa wa kwanza kutoa maudhui mtandaoni.


Akiwasilisha mada kuhusu  Kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2022, Mwanasheria  TCRA Joseph Kavishe amesema ni kosa la jinai kuendesha mtandao wa kijamii bila kusajili hivyo kuwasihi bloggers & youtubers kusajili blogs na Online Tv zao ili kuepuka mkono wa sheria huku akiwataka kulinda utu wanapoandika habari zao wakitumia lugha nzuri.

Mamlaka ya TCRA Kanda ya Ziwa imetumia kikao hicho kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari mtandaoni kuhusiana na mabadiliko madogo ya Kanuni za Maudhui Mtandao yaliyofanyika mwaka huu 2022 kwa lengo la kuboresha Kanuzi za hapo awali zilizotoka kwa mara ya kwanza mwaka 2018 chini ya Sheria ya EPOCA ya mwaka 2010.

Mabadiliko yaliyofanyika ni pamoja na kupuguza ada ya leseni kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki tano kwa mwaka na ada ya maombi kutoka shilingi laki moja hadi shilingi elfu hamsini. Lakini pia waandaaji wa maudhui yanayohusu michezo, sanaa, mapishi na elimu hawatahitaji kuwa na leseni kutoka TCRA bali leseni hiyo itatolewa kwa wale wanaotoa maudhui ya Habari (News and Current Affairs).

Meneja wa Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA), Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati akifungua kikao kazi na Watoa huduma za maudhui kwa njia ya mtandao 'Blogs & Online Tv) Kanda ya Ziwa kilichofanyika Julai 06, 2022 katika ukumbi wa TMDA jijini Mwanza.
Meneja wa Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA), Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati akifungua kikao hicho.
Mwenyekiti wa Mwanza Press Club, Edwin Soko akitoa mada kuhusu Vitisho vya Kimtandao na Ulinzi wa waandishi wa habari Mtandaoni kwenye kikao kazi cha TCRA na Watoa huduma za maudhui kwa njia ya mtandao 'Blogs & Online Tv) Kanda ya Ziwa.
Mwenyekiti wa Mwanza Press Club, Edwin Soko akitoa mada kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti Mstaafu wa Mwanza Press Club, Deus Bugaywa akitoa mada kuhusu Maadili kwa vyombo vya habari vya kimtandao.
Mwanasheria  TCRA Joseph Kavishe akiwasilisha mada kuhusu  Kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2022

Soma zaidi hapa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com