Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NGUVILA AWAHIMIZA WANANCHI KUENDELEA KUITUNZA NA KUILINDA AMANI TANZANIA


Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mh. Toba Nguvila akizungumza
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mh. Costansia Buhiye akizungumza
Viongozi wa idara mbalimbali waliohudhuria harambee hiyo

****

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewasihi wananchi wa Wilaya ya Muleba kuendelea kuienzi na kuitunza amani kwa maendeleo ya Wilaya na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza leo Julai 11, 2022 wakati wa harambee  iliyofanywa na kanisa Katoliki kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Rulondo, Kijiji cha Rwagati, Kata ya Kashasha Mhe. Nguvila amewaeleza wananchi kuwa viongozi wa Dini, viongozi wa Serikali na viongozi wa Kimila wanao wajibu wa kuhakikisha wanashirikiana kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

"Yapo matukio ya kujinyonga na ukatili wa kupiga mtu mpaka kuua, sisi kama viongozi haya mambo ni lazima tuyakemee na sisi kama waumini ni lazima tukemee hizi roho ambazo zinakwenda kinyume na mapenzi ya Mungu" amesema Mhe. Nguvila.

Aidha, amewasihi pia wananchi kuhakikisha wanaachana na tabia ya uuzaji wa kahawa kwa njia ya magendo na kuwasihi kuuza kahawa kwa njia ya mnada ambao itawasaidia wakulima wa zao la kahawa kunufaika na zao hilo.

Sambamba na hayo amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanashiriki  ipasavyo katiza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23, Agosti 2022 zoezi ambalo lengo lake ni kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Mhe. Costansia Buhiye ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi katika Harambee hiyo, amewasihi wananchi kuhakikisha wanaimarisha upendo na ushirikiano ili nchi iweze kuwa na amani.

Ujenzi wa Kanisa hilo ulianza rasmi tarehe 8/6/ 2022 ambapo mpaka sasa upo hatua ya msingi ambao umegharimu kiasi cha Tsh. Milioni 6.7 na mpaka kukamilika kwa jengo la kanisa hilo inakadiriwa kugharimu kiasi cha Tsh. Milioni 122.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com