Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU ARDHI AUNDA KAMATI KUIKABILI MIGOGORO YA ARDHI DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dkt. Allan Kijazi akiongea na vyombo vya habari kuhusu wito wake kwa wakazi wa Dare es Salaam kufika katika Ofisi ya Wizara ya Ardhi Magogoni ili waweze kupata majibu ya malalamiko na migogoro ya Ardhi ifikapo Agosti,2022 Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Waandishi wa habari waliofika ofisi za Wizara Magogoni Jijini Dar es Salaam wakisikiliza kwa makini maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Allan Kijazi wakati akitoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kufika mbele kamati yake ili waweze kupata ufumbuzi wa malalamiko yao ifikapo tarehe 1 Agosti 2022.

********************

Na Anthony Ishengoma-Wizara ya Ardhi

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi leo amekutana na vyombo vya habari Nchini kutoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufika Jengo la Wizara ya Ardhi Magogoni ifikapo tarehe 1, Agosti wafike ili waweze kutatuliwa kero na malalamiko ya ardhi yanayowakabili.

Dkt. Allan Kijazi ametoa wito huo kwa wakazi wa Dar es Salaam baada ya kuunda Kamati itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi pamoja na wataalamu kutoka Makao Mkuu Dodoma kuweka kambi ya Siku tano Dar es Salaam maalumu kwa ajili ya kushughulikia malalamiko na migogoro ya ardhi Mkoani humo.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya migogoro ya ardhi, hasa inayohusu umiliki wa viwanja kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya pamoja na jitihada za kutatua migogoro hii kwenye ngazi ya Mikoa, na Halmshauri zote Nchini.

Akiongea na Vyombo vya habari mapema leo asubuhi Dkt Allan Kijazi ameongeza kuwa Wizara ya Ardhi imebaini kwamba bado malalamiko ya wananchi yamekuwa ni mengi, na mengine ya muda mrefu na kuwakatisha walalamikaji tamaa na katika maeneo mengine kumekuwa na hali ya kuzorota kwa amani.

‘’Hili ni suala ambalo tusingependa liendelee na kutokana na unyeti wa suala la ardhi, Uongozi wa Wizara umeamua kuweka nguvu ya kipekee kwenye kutatua kero ya migogoro ya ardhi kwa kuanzia na mikoa ambayo migogoro ni mingi.’’Aliongeza Dr.Allan Kijazi.

Aidha Dkt. Kijazi ameviambia vyombo vya habari kuwa ili maboresho ya mifumo ya utendaji kazi kwenye Wizara na kupunguza kero zisiendelee kujitokeza mara kwa mara, walalamikaji wanao uhuru wa kubainisha sababu za migogoro hiyo, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Hata hivyo Dkt Kijazi amesesisitiza kuwa malalamiko yatakayofanyiwa kazi ni yale tu ambayo hayajawasilishwa mahakamani, kwa maana kwamba yasiwe kwenye mchakato wa usikiliwaji au yasiwe yameshatolewa uamuzi na Mahakama.

‘’Kwa vile zoezi hili litagusa maeneo mengi ya nchi yetu, napenda pia kuwaarifu kwamba, pamoja na hatua ambazo Wizara inachukua kutatua malalamiko na kero za wananchi wa Dar es Salaam, tunaelewa kwamba jukumu letu la msingi ni kujenga utaratibu na mifumo ya kuzuia migogoro isijitokeze, na sio kusubiri migogoro ijitokeze ndio tuanze kuifanyia kazi.’’Aliongeza Dkt.Kijazi Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.

Aidha Katibu Mkuu Kijazi alisema hoja na malalamiko yatakayowasilishwa, kamati itakayosikiliza kero itafanya uchambuzi wa kina kubaini sababu za malalamiko kuwa mengi, na kupendekeza hatua muafaka.

‘’Napenda pia kuwafahamisha kwamba, taarifa ya Kamati ya kubaini sababu za malalamiko itakuwa sehemu ya hatua ambazo Wizara imeanza kuchukua kufanya maboresho ya utaratibu na mifumo ya utoaji huduma ili kupunguza usumbufu na malalamiko ya wateja.’’Aliongeza Dkt Kijazi.

Dkt Kijazi alizitaja hatua zitakazochukuliwa kutatua migogoro ya ardhi kuwa ni kuwa na ofisi ya pamoja ya utoaji huduma kwa wananchi wanaohitaji huduma za ardhi kuanzia tarehe 01 Agosti 08, 2022.

Akitoa ufanunuzi juu ya hatua hiyo muhimu Dkt Kijazi alisema hii inamaanisha kwamba, mwananchi anayehitaji huduma anaweza kupata huduma kwa uwepo wa taarifa zote zinazohusu masuala ya michoro ya mipango miji kwamaeneo yanayohusu, taarifa za upimaji, na kumbukumbu muhimu za kumsaidia kupata hati.

Dkt Kijazi aliitaja hatua nyingine kuwa ni kuandaa Mwongozo ambao utakuwa na Vigezo na Utaratibu wa Kutathimini na Kupima Misingi ya Utawala Bora kwenye Sekta ya Ardhi.

Aidha Mwongozo huu utasaidia kuweza kubaini viashiria vya ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwenye kila hatua ya utoaji maamuzi yanayohusu masuala ya ardhi.

Kwa siku za karibuni, Serikali iliweka nguvu kwenye kutafuta ufumbuzi wa changamoto za migogoro mikubwa, na ili kufanikisha zoezi hili Mh Rais aliunda Kikundikazi cha Mawaziri wa kisekta ili kutekeleza maamuzi ya Baraza ya Mawaziri kuhusu migogoro hiyo 975 mikubwa ambayo ilishafanyiwa kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com