Na Mwandishi Wetu,MPANDA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-Bara), Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amewataka wanawake na vijana nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi za ungozi ndani ya Chama na kuwahakikishia kuwa haki itatendeka huku akisema hakuna wa kumtisha mwenzake.
Kinana ameyasema hayo leo mjini Mpanda mkoani Katavi, wakati akizindua mradi wa fremu 15 za maduka zilizojengwa katika Ofisi za CCM za mkoani humo, ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM.
Akifafanua zaidi Kinana alisema, uchaguzi ndani ya Chama upo katika hatua mbalimbali hivyo ni vyema wana CCM wakajitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili kuwania nafasi za uongozi.
"Niwaombe akina mama mkachukue fomu msiogope, nendeni mkachue fomu mpambane na wanaume.
"Nataka niwasihi vijana gombeeni hizo nafasi, uchaguzi ukija nafasi zitakuwa wazi na kila mtu anahaki sawa na mwenzake, hakuna masultani wa kukaa madarakani milele, tuna uchaguzi kila baada ya miaka mitano, wenye kuwachagua viongozi ni wana CCM, wakikupenda, wakikuheshimu na wakithamini mchango wako watakupa kura, wasipothamini watakunyima kura.
"Nafikiri na ninyi mnawafahamu wajumbe sio watu wazuri, wanaweza kukwambia usiwe na wasiwasi tutakupa kura, halafu baadae unatoka kapa, hivyo niwaombe sana vijana gombeeni, kina mama gombeeni, tutatenda haki, hatutampendelea mtu, wala mtu asimtishe mwenzake, kwamba ukienda kuchukua fomu unaambiwa na wewe unatafuta nini, kwani na wewe ulivyochukua fomu mwingine sialikuwepo kabla yako, ndio umechukua nafasi yake na mimi nakuja kukung'oa wewe," amesema