FARIDAH Kiconco (37); ni mama aliyeambiwa kwenye kituo cha afya kuwa ana Virusi Vya Ukimwi (HIV) kisha akatumia dawa kwa miaka sita, kumbe hana Ukimwi.
Faridah amefungua kesi akidai fidia baada ya dawa alizopewa kunywa kwa miaka hiyo kumletea matatizo ya kiafya kwenye figo na ini.
Faridah, raia wa nchini Uganda, akihojiwa kwa masikitiko amesema, mwaka 2011 alikwenda kituo cha afya cha Kabwohe kupima mimba, lakini pia akaambiwa apime na Virusi Vya Ukimwi ambapo majibu yalikuja akaambiwa ameathirika hivyo akapewa dawa za kuanza kutumia.
Anasema mwaka 2012 alijifungua mtoto wake wa kwanza na 2017 akajifungua mtoto wake wa pili, lakini mwezi mmoja tu baada ya kujifungua mtoto wa pili, ngozi yake ikaanza kubadilika rangi kuwa ya njano.
Anasema alirudishwa kituo husika cha afya kisha baadaye alikwenda Hospital ya Rufaa ya Mbarara ambapo huko alifanyiwa vipimo upya kwa kina na kuonekana hana Virusi Vya Ukimwi bali ogani zake muhimu figo na ini hazifanyi kazi vizuri kama kawaida na sababu ikiwa ni dawa hizo za Virusi Vya Ukimwi alizopewa kutumia kwa miaka 6 kuanza kumletea madhara (side effects).
Mwaka 2018 alifungua kesi dhidi ya Serikali kuhusu kituo husika cha afya kumsingizia kuwa ameathirika ambapo hadi sasa takriban miaka 4 kesi haijasikilizwa hata mara moja licha ya kuwa ilifika mahakamani tangu muda huo.
Kituo husika kilichompakazia Faridah kuwa ana ‘ngoma’, daktari alipoulizwa amesema yeye ni mgeni hapo kikazi ana miezi tu, hajui kilichotokea muda huo kwani hakuwepo.
Kwa upande wa mahakama wanasema jaji husika aliyekuwa asikilize kesi hiyo alistaafu hivyo anasubiriwa jaji mwingine.
Stori: Sifael Paul
Global Publishers
Social Plugin