Waziri wa Nishati January Makamba akiongea na wakazi wa kijiji cha Ugaka, kata ya Ugaka katika Jimbo la Manonga wilayani Igunga Mkoani Tabora ambapo aliahidi kumpatia sh mil 50 kijana Sori Gelard mkazi wa kijiji hicho ili kuanzisha mradi wa ujenzi wa kituo cha mafuta kijijini hapo, pia aligawa mitungi 50 ya gesi ya kupikia kwa ajili ya kusaidia akinamama ili kuepukana na matumizi ya kuni ambapo moshi umekuwa akiathiri sana afya zao na kupelekea kupiteza maisha.
***
SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati inatarajia kuanza kutoa mikopo nafuu ya sh mil 40 kwa wakazi wa vijijini wenye uwezo wa kuanzisha vituo vya kuuzia mafuta ya vyombo vya moto ili kurahisisha upatikanaji huduma hiyo vijijini.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Nishati January Makamba alipokuwa akiongea na wakazi wa kata ya Choma na Ugaka katika Jimbo la Manonga Wilayani Igunga Mkoani hapa.
Alisema wakazi wa vijijini wamekuwa wakipata shida wanapohitaji huduma ya mafuta ya petroli, diseli au ya taa na hata wakiyapata wanatumia gharama kubwa kuyanunua na yanakuwa yameshachakachuliwa.
Alibainisha kuwa serikali imekuja na mkakati wa kurasimisha biashara hiyo kwa wakazi wa vijijini kwa kuwawezesha na kupata mafuta halali yasiyochakachuliwa, na kuongeza kuwa wanatarajia kuanza kutoa mikopo nafuu ya sh mil 40 kwa wana vijiji wenye uwezo wa kupata maeneo ya kujenga vituo hivyo.
‘Tumelegeza masharti kwa wanavijiji wote wanaotaka kuanza kuuza mafuta, tutawawezesha mikopo nafuu ya kujenga vituo hivyo ili kuanza kutoa huduma hiyo kwa wananchi wenzao wa maeneo ya vijijini’, alisema.
Waziri Makamba alifafanua kuwa wataweka utaratibu mzuri ambapo halmashauri za wilaya zitasimamia zoezi hilo kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na wote watakaohitaji mikopo hiyo wataomba kupitia halmashauri.
Ili kuonesha dhamira njema ya serikali kuanzisha mpango huo, Waziri aliahidi kumpatia kijana anayeuza mafuta ya petrol ya kupima Siro Gerald mkazi wa kijiji cha Ugaka kiasi cha sh mil 50 ili kutoa mfano kwa wanakijiji wengine kuanzisha mradi huo.
Aliongeza kuwa serikali imetenga sh bil 2 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili kutekeleza mpango huo, kwa sasa wanandaa utaratibu mzuri utakaosaidia kufanikisha utekelezaji wake.
Mpango huo uliungwa mkono na Mbunge wa Jimbo la Manonga Seif Gulamali na kubainisha kuwa utasaidia wakazi wengi wa vijijini kujiongezea kipato hivyo kujikwamua kiuchumi.
Alishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya afya, maji, barabara na umeme katika mkoa huo na mikoa yote nchini na kuomba vijiji vyote kuunganishiwa huduma ya umeme wa REA ili kuboresha maisha yao.
Akitoa neno la shukrani kijana Siro alimhakikishia Waziri kuwa amepokea ahadi hiyo kwa mikono miwili na kwamba fedha hizo atazitumia vizuri kujenga kituo hicho ili kujikwamua kiuchumi.