Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, akipokea maelezo kutoka kwa Mkaguzi wa Afya ya Mazingira wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, kuhusiana na ukaguzi wa mazingira ya kazi ambao hufanywa na OSHA.
Naibu Waziri wa OSHA, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, akipata elimu kutoka kwa Mkaguzi wa Afya ya Mazingira wa OSHA, Bw. Simon Lwaho kuhusu ukaaji sahihi katika dawati la kazi.Kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usajili wa OSHA, Bi.Yolanda Mbatiya juu ya namna ambavyo mfumo wa kimtandao wa kusajili maeneo ya kazi wa WIMS umerahisisha huduma ya usajili wa miradi na maeneo ya kazi kwa wadau wa OSHA.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, akipata elimu kutoka kwa Wakaguzi wa Afya wa OSHA kuhusu vipimo mbalimbali vinavyotumiwa na wataalam wa OSHA katika zoezi la uchunguzi wa afya za wafanyakazi katika maeneo ya kazi.
Timu ya Maonesho ya OSHA ikiongozwa na Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda wakimhudumia mdau aliyetembelea banda la Maonesho la OSHA.
****************************
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amewataka wamiliki wote wa maeneo ya kazi kuhakikisha kwamba wanasajili maeneo yao ya kazi na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ili Taasisi hiyo iweze kuwafikia na kuwapa huduma za ukaguzi na ushauri kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.
Ametoa agizo hilo baada ya kuhitimisha ziara katika Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo OSHA zilizokuwa zinashiriki maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ambapo alipokelewa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.
“Suala la msingi zaidi ninalolisisitiza hapa ni kwa wamiliki wa sehemu za kazi ama waajiri kuendelea kujisajili katika Taasisi ya OSHA ili waweze kufanyiwa ukaguzi wa maeneo yao ya kazi katika kutekeleza Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi. Ni wajibu wa serikali na waajiri wote kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi yanakuwa salama na kazi zinazofanyika zinakuwa zenye staha ambapo suala hili linaanza na kuwa na afya njema kwani afya ndio mtaji namba moja katika uzalishaji,” amesema Naibu Waziri Katambi na kuongeza:
“OSHA wamekuwa wakiendelea kusimamia kazi hii vizuri na wamekuwa wakihakikisha wakati wote wanatembelea maeneo ya kazi kwa ajili ya kufanya ukaguzi ili kutambua maeneo hatarishi na kisha kutoa maelekezo na miongozo juu ya namna sahihi za kuwakinga wafanyakazi kwa mujibu wa sheria na kuwachukulia hatua stahiki wale wanaokaidi maelekezo ya serikali.”
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema jukumu kuu la Taasisi yake ni kuwezesha biashara na shughuli mbali mbali za uwekezaji nchini ili shughuli hizo ziweze kuwa na tija.
“OSHA ni Taasisi wezeshi na kama inavyofamika dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha kwamba inakuza biashara na uwekezaji nchini hivyo sisi tumeangalia nini tunaweza kufanya katika kufanikisha dhamira ya serikali na tukaona tuondoe tozo takribani 13 zenye thamani ya zaidi ya bilioni 35 ambazo kama zingeingia katika mfuko mkuu wa serikali zingeenda kujenga barabara, mashule hospitali nakadhalika lakini Mheshiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia fedha hizi kubakia mikononi mwa wawekezaji ili zikaboreshe mifumo ya kuwalinda wafanyakazi,” amesema Mwenda.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye jukumu la kusimamia Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama na Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba shughuli zote za uzalishaji nchini zinafanyika kwa kuzingatia taratibu za afya na usalama ili kulinda nguvukazi na mitaji ya wawekezaji.
Social Plugin