Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ASHTUKIA AJIRA ZA POLISI...BAADHI YA POLISI HAWANA SIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

RAIS wa Jamhuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema atakwenda kuuchunguza mfumo wa ajira katika majeshi ya ulinzi nchini akieleza kuwa wanaoajiriwa kwani inaonekana baadhi yao hawana uwezo na sifa za kuyatumikia majeshi hayo.


Rais Samia amesema hayo leo Jumatano, Julai 20, 2022 wakati akithutubia mara baada ya kumaliza kumwapisha Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura.


“Eneo jingine muhimu ni mfumo wa ajira, mafunzo na nidhamu lazima tukalitazame katika vyombo hivi vya haki jinai. Haki za watu lazima tuzipe kipaumbele. Lazima tukatazame mifumo ya utendaji kazi kama sharia zetu zinavyotaka.


“Tutaangalia watenda kazi wanapatikanaje? Sifa za watenda kazi. Kuna wakati nilikuwa namtania Sirro (IGP aliyemaliza muda wake), embu niambie, ukienda Jeshini kule unaambiwa waliingia 200 lakini 50 walishindwa, wengine walipotoka nidhamu tukawasimamisha, mbona chuoni kule Moshi sijawahi kusikia kwamba hawa wamerudishwa?


“Sirro akaniambia afande wapo, wapo bwana wapo. Lakini kwa kweli nadhani tukatazame vizuri huko, kwa sababu vitendo vinavyofanywa na polisi barabarani unashindwa kuelewa huyu mtu alihitimu mafunzo vizuri kweli?


“Lakini background wanazoingilia jeshini, tukipekuana huko unakuta feki nyingi tu chungu nzima, kwa hiyo inawezekana hata uwezo wa huyo mtu anapelekwa kwenye hayo mafunzo hana uwezo, lakini husikii karudishwa.


“Kwa hiyo tutakwenda kupekuana huko kujua upatikanaji wa watenda kazi, majeshi yote tunakwenda kutazama vizuri huko, tutachujana vizuri sana ili kujenga majeshi yenye hadhi na sifa ya kuisimamia nchi hii.


“Pia, tutaangalia wataalam wabobezi, je, tunapoajiri wapo? Nafahamu majeshi yetu yanahitaji mainjinia, wataalam wa afya, watalaalam wa fedha, watalaam wa ICT, lakini je ndio tunaowaajiri? Na kama wapo, wanatosheleza? Sifa zao mpaka leo ndio zenyewe?” amesema Rais Samia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com