Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS WA KOFIH AFANYA ZIARA MLOGANZILA

Rais wa Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH) Prof. Chang-yup Kim akisaini kitabu cha wageni alipofanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kutembelea miradi iliyofadhiliwa na taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Prof. Lawrence Museru akimuelezea Raisi wa KOFIH namna gani miradi hiyo ilivyosaidia kuboresha huduma za afya hospitalini hapo.Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akisoma taarifa fupi mbele ya Raisi wa KOFIH na kuelezea miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na taasisi hiyo.Prof. Kim akielezea namna alivyofurahishwa na uongozi wa MNH-Mloganzila pamoja na usimamizi mzuri katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.Baadhi ya wakurugenzi wakimsikiliza Dkt. Magandi akisoma taarifa fupi mbele ya Raisi wa KOFIH.Prof. Kim na Prof. Museru pamoja na baadhi ya wakurugenzi wakitembelea baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na KOFIH.Prof. Museru na Dkt. Magandi wakimkabidhi Raisi wa KOFIH zawaidi ya kinyago cha Umoja ikiwa ni ishara ya kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya taasisi ya KOFIH na Hospitali ya Mloganzila

**************************

Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH) imesema itaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano baina ya taasisi yake na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ili kuendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa KOFIH Prof. Chang-yup Kim alipofanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kutembelea miradi iliyofadhiliwa na taasisi hiyo.

Prof. Kim amesema KOFIH itaendelea kutoa kipaumbele kwa kuwajengea uwezo wataalamu katika fani mbalimbali kwa kuamini kuwa endapo watapata mafunzo na ujuzi wa kutosha huduma za afya zitaendelea kuwa bora na kukidhi mahitaji ya wananchi.

“Tunaamini kwa usimamizi huu mzuri na uendeshaji wa hospitali chini ya Prof. Museru, hospitali hii itaendelea kuwa bora zaidi kwa utoaji huduma hapa nchini”amesisitiza Prof. Kim.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji MNH- Mloganzila, Prof. Lawrence Museru ameishukuru KOFIH kwa kuendelea kuisaidia hospitali hii katika maeneo mbalimbali ikiwemo vifaa tiba, mafunzo, utafiti na miundombinu.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Korea Kusini kupitia mashirika yake ya KOFIH na Africa Future Foundation kwani wamekuwa wafadhili tunaowategemea kwa kiasi kikubwa katika kuendelea kuboresha huduma katika hospitali hii” amesema Prof. Museru

Pamoja na hayo, ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini hususani huduma ya afya ya mama na mtoto, ununuzi na usimikaji wa mashine za MRI, CT Scan na X-ray kwa baadhi ya hospitali hapa nchini.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi ametaja baadhi ya miradi ambayo imefadhiliwa na KOFIH kuwa ni pamoja na ujenzi na usimikaji wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba.

“Misaada hii imekuwa na faida kubwa sana katika hospitali yetu kwa mfano mradi wa uzalishaji wa hewa tiba umeweza kuokoa takribani TZS 33 Mil ambazo zingetumika endapo hospitali ingenunua hewatiba kutoka kwa wazabuni mbalimbali” ameongeza Dkt. Magandi.

Amefafanua kuwa miradi mingine iliyofadhiliwa na KOFIH ni pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto ambao umehusisha ukarabati wa wodi ya watoto wachanga walio katika uangalizi maalum, kuanzisha wodi ya mama wajawazito walio chini ya uangalizi maalum na ukarabati wa karakana ya vifaa tiba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com