WADAU wa sekta za biashara na usafirishaji wameitaka serikali kutoipa kampuni ya TICTS mkataba mpya wa kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam kwa kushindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka na kushindwa kuwekeza kwenye miundombinu ya bandari.
Kusuasua kwa TICTS kumeongeza gharama ya kuingiza mizigo nchini na kulikosea taifa mapato ya trilioni ya Shilingi kutokana na wafanyabiashara wa nchi jirani kuamua kuikwepa bandari ya Dar es Salaam na kukimbilia bandari za Kenya, Afrika Kusini na Namibia zenye ufanisi zaidi.
Chama wa Mawakala wa Forodha (TAFFA) kimelalamika mara kadhaa kuhusu TICTS kuwa na ufanisi mdogo na kusababisha ucheleweshaji wa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Wabia wa TICTS ni pamoja na waziri wa zamani Nazir Karamagi na mfanyabiashara maarufu Yogesh Manek, wakishirikiana na mwekezaji wa nje, kampuni ya Hutchinson Ports ya Hong Kong.
Taarifa kutoka bandarini zinaonesha kuwa TICTS walipewa nyongeza ya mkataba wa miaka mitano mwaka 2017 baada ya kushindwa kuleta ufanisi tangu wapewe kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Kuna juhudi zinaendelea ili TICTS waongezewe mkataba mwingine wa miaka mitano licha ya kushindwa kuleta ufanisi kwa zaidi ya miaka 20.
Takwimu za serikali zinaonesha kuwa TICTS walihudumia makontena ya futi 20 (TEUs) 606,169 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.8 tu kulinganisha na mwaka 2020.
TICTS wameshindwa kufikia lengo la kimkataba la kuongeza mzigo wa kontena kwa asilimia 37 kwa mwaka l.
Wakati TICTS inasababisha bandari ya Dar es Salaam ikose ufanisi, bandari ya Mombasa nchini Kenya inaelekea kuwa bandari kitovu yenye kupitisha makontena ya TEU milioni 2 kwa mwaka.
Wakati huo huo, bandari ya Durban nchini Afrika Kusini ina mpango wa kukuza mzigo wa kontena hadi kufikia TEU milioni 11 ndani ya miaka michache ijayo.
"Serikali isiwape TICTS mkataba mpya tena kwani wameshindwa kazi kwa miaka 20 sasa," alisema John Tarimo, mfanyabiashara wa Dar es Salaam anayeagiza bidhaa kutoka China.
"Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kutoa mkataba wa kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam kwa kampuni nyingine kubwa ya kimataifa ilete tija."
Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa haridhishwi na ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam na akamtengua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi. Nafasi yake imechukuliwa na Plasduce Mbossa ambaye ameahidi kuongeza ufanisi wa bandari.
Social Plugin