Afisa Uhusiano na huduma kwa Wateja kutoka Shirika la TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma,akizungumza na wananchi wa Kata ya Mnadani wakati akihamasisha pamoja na kutoa elimu kwa wananchi watakaonufaika na miradi ya REA jijini Dodoma.
Afisa Usalama TANESCO Mkoa wa Dodoma Bw.Madega Dudu,akiwatahadharisha kwa wananchi dhidi ya utapeli na uhujumu miundombinu ya umeme Katika maeneo yao wakati wakiendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Mnadani watakaonufaika na miradi ya REA jijini Dodoma.
Diwani kata ya Mnadani Paul Bakinye ,akiishukuru TANESCO Mkoa wa Dodoma kwa kufika Katika kata yake kwa ajili ya kuhamasisha na kutoa elimu juu ya Miradi ya REA katika jiji la Dodoma.
Mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo Jijini Dodoma Marlon Bulugu,akielezea hatua za mradi zilipofikia wakati wa zoezi la kuhamasisha na kutoa elimu juu ya Miradi ya REA katika jiji la Dodoma.
WANANCHI wa Kata ya Mnadani wakiendelea kupata elimu juu ya Miradi ya REA katika jiji la Dodoma ikitolewa na Afisa Uhusiano na huduma kwa Wateja kutoka Shirika la TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma (hayupo pichani)
....................................
Na Alex Sonna-DODOMA
SHIRIKA la umeme nchini TANESCO Mkoa wa Dodoma linaendelea na uhamasishaji na utoaji Elimu maeneo yanayonufaika na miradi ya REA jijini Dodoma ambapo kufikia mwisho wa awamu hii ya miradi wananchi zaidi ya 30,000 wanatarajiwa kufikiwa na huduma.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mnadani,Afisa Uhusiano na huduma kwa Wateja Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma , amesema kuwa miradi hiyo ya REA imelenga kujaziliza na kufikia maeneo yote ambayo umeme ulipita bila kusambazwa awamu zilizopita pamoja na kufikia maeneo ya pembezoni mwa Jiji.
"Kata ya Mnadani ni kata iliyonufaika na miradi miwili ya REA ile ya ujazilizi na ya pembezoni, ambayo umeme umeshawashwa na tunategemea kuunganisha wateja zaidi ya 350 kwenye kata hii". Amesema Libogoma
Ameongezea kuwa, pamoja na umeme kufika majumbani ni vyema wananchi walio eneo la mradi wakachangamka na kutumia fursa ya miradi hii kuweza kukuza uchumi binafsi na ule wa maeneo yao kwa kuomba huduma ya umeme mapema.
" Shirika limeboresha taratibu za uombaji huduma kwani sasa hakuna mambo ya fomu, kwa kutumia namba yako ya Nida utaomba umeme moja kwa moja TANESCO kupitia NiKONEKT ambapo kama una simu janja utapakua Nikonekt na kufanya maombi au kama ni kitochi utabonyeza *152*00# na kisha kufuata maelekezo ya kufanya ombi lako, hatuna mawakala wanaosajili maombi mtaani tafadhali tuepuke vishoka..."
Kwa upande wake Afisa Usalama TANESCO Mkoa wa Dodoma Bw.Madega Dudu,amewatahadharisha wananchi dhidi ya utapeli na uhujumu miundombinu ya umeme Katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika utoaji wa taarifa za wazi na siri kwa TANESCO ili hatua zichukuliwe mapema.
"Mpaka umeme huu wa unafikishwa hapa umesafiri kutoka mbali sana na umepita katika njia salama ndio maana unawaka, hivyo ni jukumu mojawapo la sisi Wanambwanga na Wanandachi kiujumla kulinda miundo mbinu iliyopo hapa na kuhakikisha usalama muda wote kwani Shirika linaendelea na kubaini wahujumu na kuwachukulia hatua kama ambavyo sheria ya uhujumu inavyotaka", amesema Dudu
"Kumekuwa na wizi wa nyaya za umeme aina ya shaba ambazo zinafungwa kwenye mashine umba (Transformer) ambazo zimewekwa kwaajili ya ulinzi wa miundo mbinu ili kuepusha madhara lakini kumekuwa na watu ambao wamekosea uzalendo wanakata na kuiba zile nyaya na kuturudisha nyuma, kwaio ulinzi shirikishi ni muhimu kulinda hii miundo mbinu". amesema Dudu
Naye Mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo Jijini Dodoma Marlon Bulugu, amesema mradi kwa sasa upo ukingoni kazi inayoendelea ni kukamilisha uvutaji nyaya sehemu iliyobakia.
"Wiki lijalo tunakamilisha kazi ya uvutaji nyaya kwa nguzo zilizobakia, tunachohitaji ni muitikio wenu hivyo ni vyema wananchi mkaendelea na maombi ili nasi tuweze kukamilisha ufungaji mita mapema katika nyumba zenu".amesema Bulugu.
Naye Diwani kata ya Mnadani Paul Bakinye ameishukuru TANESCO kwa kufika Katika kata yake na kuelewesha wananchi wa mitaa yake juu ya miradi ya umeme na matarajio ya serikali kwenye kata yake kupitia miradi hii.
Uelimishaji huu unaendelea mtaa kwa mtaa mjini Dodoma katika kata zote zinazonufaika na miradi hii.
TANESCO Dodoma inasimamia utekelezaji wa miradi miwili ya REA inayoendelea ndani ya Jiji la Dodoma, miradi hii ni ya ujazilizi unaotekelezwa na mkandarasi Derm Electrics na ile ya pembezoni (peri-urban) unaotekelezwa na mkandarasi Cylex Engineering.
Mpaka sasa miradi hii imefikia 91% na 79% za utekelezaji wake ambapo tayari wateja zaidi ya 18,000 Mkoa mzima wamekwisha unganishiwa huduma.
Social Plugin