Na Mwandishi Wetu, Johannesburg, Afrika Kusini
Timu tatu za Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zimejishindia zawadi za pili na tatu katika Shindano la TEHAMA la sita la Huawei Duniani ambalo lilifikia tamati Juni 25 mwaka huu Johannesburg, Afrika Kusini. Huo ni ushindi wa pili kwa Tanzania kwa miaka miwili mfululizo.
Kwasasa Huawei inashirikiana na vyuo vikuu 18 vya juu nchini Tanzania kuanzisha vyuo vya TEHAMA, ikipanga kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi zaidi ya 1000 kila mwaka. Hivi sasa, takriban wanafunzi 5,000 wamepatiwa mafunzo.
Akizungumzia mafanikio hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe alipongeza juhudi za wanafunzi na mipango ya Huawei katika kukuza vipaji vya wanafunzi wa Kitanzania.
‘’ Nawapongeza wanafunzi wa Tanzania kwa kushinda shindano la TEHAMA la Huawei, kama serikali tunajivunia wanafunzi hawa kwa ufaulu huo mkubwa. Ushindi huu unathibitisha ubora wa kitaaluma wa vyuo vikuu vyetu kwa kiwango cha kimataifa. Natumai Shindano la TEHAMA Huawei linaendelea kutafuta na kutoa mafunzo kwa vipaji zaidi vya TEHAMA nchini Tanzania. Ningependa kuwashukuru Huawei kwa kujitolea na juhudi katika kujenga mfumo wa ikolojia wa vipaji vya ndani" alisisitiza.
Timu za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zilifanya vyema kati ya washiriki 130 wa fainali za kimataifa, na kushinda tuzo 18 (2 Tuzo kuu, Zawadi 4 za Kwanza, Zawadi 4 za Pili na 8 za Tatu), na kuwa eneo lenye timu zilizoshinda tuzo nyingi zaidi.
Timu mbili kutoka Nigeria zilishinda tuzo kuu, ikiwa ni ushindi wa pili kwa Nigeria katika michuano ya kimataifa. Timu nyingine mbili za Nigeria zilishinda tuzo ya kwanza na zawadi ya pili. Timu kutoka Uganda na Kenya zilijinyakulia zawadi ya kwanza, timu kutoka Tanzania na Ghana zilijinyakulia zawadi ya pili, na timu za Zimbabwe, Mauritius, Tanzania, Kenya, na Ghana zilijinyakulia zawadi ya tatu.
Shindano hilo la TEHAMA ni sehemu muhimu ya mpango wa “LEAP”, programu ya kukuza mfumo wa ikolojia ya vipaji iliyozinduliwa na Huawei katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mpango huu unalenga kuibua zaidi ya vipaji 100,000 vya TEHAMA katika ukanda huo ndani ya miaka mitatu. Kupitia kuandaa mafunzo ya ustadi wa kidijitali, na kuwatia moyo wanafunzi kushiriki katika mashindano ya ujuzi husika, LEAP imejitolea kuboresha ujuzi wa kidijitali wa vijana katika eneo hili na kukuza ushindani wa ajira. Husaidia kukidhi hitaji kubwa la talanta dijitali katika biashara na jamii.
Shindano hilo lilivutia wanafunzi 150,000 kutoka nchi 85. Baada ya mwaka wa michakato ya uteuzi, timu 130 zilifika fainali ya kimataifa. Kiwango cha shindano hilo kilikuwa kikubwa zaidi kuwahi kutokea. Miradi ya shindano ilijumuisha suluhu za ubunifu za wingu, mtandao, na dijitali, ambayo inawahimiza wanafunzi kuchanganya maarifa yao ya TEHAMA na mazoezi yao na kupendekeza masuluhisho ya kibunifu ili kushughulikia matatizo yanayokabili maendeleo ya kijamii.