Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Henry Mwaibambe aliyefika eneo la tukio amesema ajali hiyo iliyotokea Agosti 8,2022 Majira ya saa nne kasoro usiku katika kijiji cha Mwakata kata ya Mwakata wilaya ya Kahama katika barabara kuu ya Isaka – Kahama imehusisha magari manne kugongana na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa vyombo hivyo vya usafiri.
"Ajali ilihusisha gari lenye namba za usajili T880 DUE Toyota IST iliyokuwa inatokea Isaka kuelekea Kahama, iliigonga kwa nyuma trekta yenye namba T719 AUP ikiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika na kusababisha vifo vya watu watatu waliokuwa kwenye gari ya IST.
"Wakati huo imeshatokea ajali nyingine eneo hilo hilo kwenye barabara hiyo ambapo ajali ya pili ilihusisha gari la Hiace yenye namba T350 BDX ikiendeshwa na Salinja Lukelele (28) ikitokea Kahama kuelekea Isaka iliigonga kwa mbele gari yenye namba T658 DUW Scania ikiendeshwa na dereva ambaye bado hajapatikana na kusababisha vifo vya watu 13 waliokuwa kwenye hiyo Hiace",amesema Kamanda Mwaibambe.
"Hiyo Scania ilikuwa imepaki na huyo dereva wa Hiace akitokea huko alijua kabisa pale kuna ajali na kuna baadhi ya magari yalikuwa yamesimama lakini yeye akawa anafanya jitihada za kukwepa magari yaliyosimama ili awahi kule anakotaka kwenda matokeo yake akaenda kuivaa hiyo Scania.
“Kwenye hiyo IST waliofariki ni wanaume, uchunguzi wa awali unaonesha hiyo gari ilikuwa kwenye mwendo kasi imeharibika, iliingia chini ya Trekta, huenda dereva alikuwa amelewa kwani tumekuta pombe aina ya Kvant ndani ya gari”, ameongeza Kamanda Mwaibambe.
Amesema Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama na majeruhi wanaendelea kupata matibabu.
“Ukiangalia muktadha wa hii ajali ni ajali ya uzembe mkubwa sana, hili trekta lilibeba kuni nyingi na halikuwa na Reflector, lakini pamoja na kwamba hii trekta haina reflector lakini IST ina taa aliingiaje chini ya trekta, mwenye IST na trekta wote wana makosa.
“Ajali ya pili nayo dereva wa Hiace anajua kabisa kuna ajali na magari yamesimama lakini anatoka mbio kuyapita magari hayo,huyu mwenye Scania aliona gari inayumba yumba kwa speed akapaki yeye akaivaa Scania",amesema.
Amewasisitiza watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za barabarani.