Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (wa tatu kulia) akibonyeza kitufe kuashiria kufunguliwa rasmi kwa wiki ya AZAKI 2022 katika hafla iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2022 leo Agosti 18, Jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutoka Ofisi ya Rais (OR TAMISEMI) Linus Kahendagaza akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (wa tatu kusho) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS) Francis Kiwanga (wa pili kushoto) pamoja na Mratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Linus Kahendagaza (wa pili kulia) katika uzinduzi rasmi wa Wiki ya AZAKI uliofanyika leo Agosti 18,2022 Jijini Dar es Salaam. (wa kwanza kushoto) ni, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Lilian Liundi, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM Nesia Mahenge.
Mratibu wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Justice Rutenge, akizungumza katika hafla hiyo kuelezea matukio mbalimbali yatakayofanyika katika Wiki AZAKI ya 2022 yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 24, 2022 mpaka Oktoba 28, 2022.
Na: Mwandishi wetu,DAR ES SALAAM.
Imeelezwa kuwa jitihada za makusudi zinazofanywa na Asasi za kiraia katika kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo zinatambuliwa na sekta binafsi kama sehemu muhimu ya kuharakisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 18,2022 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela katika uzinduzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2022 ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Nsekela amesema kuwa ushirikiano baina ya aAasi za kirais na Sekta Binafsi unaweza kutoa suluhisho la changamoto za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ufanisi zaidi kuliko kila Taasisi kufanyakazi kivyake.
"Kwa bahati mbaya kumekuwepo na ushirikiano usioridhisha kati ya Asasi za kiraia na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto za kimaendeleo nje ya ushirikiano wa kiufadhili. Hata hivyo, sisi ni wamoja. Ushirikiano kati ya sekta mbalimbali miongoni mwa mashirika, taasisi na wananchi ni miongoni mwa hatua zinazohitajika kuchukuliwa. Tunajenga Taifa moja na jamii moja ya kimataifa. Tunajenga simulizi zetu kwa ajili ya maendeleo yetu" amesema Nsekela.
Na kuongeza kuwa "Katika Sekta Binafsi tunaongelea uwekezaji unaoleta matokeo chanya. Huu ni uwekezaji unaofanywa kwa lengo la kuleta matokeo ya kijamii au kimazingira yanayopimika mbali na faida za kifedha. Lengo ni kuleta maendeleo ya kijamii na uthabiti wa kiuchumi. Msisitizo wa uwekezaji wenye kuleta matokeo chanya kijamii ni msingi muhimu wa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya sekta binafsi na asasi za kiraia. Hii pia inaakisi Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Malengo Endelevu ya Maendeleo” ameongeza Nsekela.
Wiki ya Asasi za Kiraia ya 2022 inawaleta pamoja washirika muhimu wa maendeleo na ina lengo la kuimarisha ushirikiano wenye lengo la kukuza ushiriki wa Asasi za kiraia katika maendeleo ya Tanzania, kuimarisha hatua za pamoja zenye lengo la kufanyia kazi changamoto za kimaendeleo na kubadilishana mawazo kuhusu changamoto hizo.
Kuhusu Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Nsekela amesema, “Tunaisubiri kwa hamu Wiki ya Asasi za kiraia ya mwaka huu. Tujikite zaidi katika kuoanisha uwekezaji wa Sekta Binafsi na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. Uwekezaji wenye kuleta matokeo chanya ya kijamii ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta maendeleo endelevu.”
“Tusherehekee maendeleo ya watu kupitia simulizi za mabadiliko yaliyofanikishwa kwa kiasi kikubwa na Asasi za kiraia, lakini pia tuje na njia mpya za kuwekeza katika mipango ya kijamii kupitia ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga, amezungumzia kwa ufupi historia ya Wiki ya Asasi za Kiraia.
“Ujumbe wa mwaka 2018 ulikuwa ni ‘Ukuzaji wa Viwanda Tanzania: Watu, Sera na Utekelezaji’. Mwaka 2019 ujumbe ulikuwa ni ‘Maendeleo Kupitia Ushirikiano: Ushirika Kama Chachu ya Maendeleo Tanzania’, na mwaka 2021 ulikuwa ni ‘Mchango wa Asasi za Kiraia kwa Maendeleo ya Taifa’. Tangu kuanzishwa kwake, kumekuwa na utambuzi unaoongezeka miongoni mwa wadau wa umuhimu wiki hii kama jukwaa muhimu linalowakutanisha wadau mbalimbali. Sisi sote ni mashahidi wa umuhimu na matokeo chanya ya Wiki ya Asasi za Kiraia tangu ilipoanzishwa, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa umoja na mshikamano miongoni mwa wadau wa maendeleo nchini. Wiki ya Asasi za Kiraia pia imeleta mwamko mkubwa miongoni mwa washirika wa maendeleo wa umuhimu wa kuionyesha jamii mchango wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Wiki hii huweka msisitizo katika umuhimu wa ufanyaji kazi wa pamoja na ushirikiano katika kuwafikia wananchi,” alisema.
Naye Mratibu wa Wiki ya Asasi za Kiraia, Justice Rutenge, amesema ajenda ya wiki ya mwaka huu itajikita katika kuhakikisha washirika katika sekta mbalimbali wanakuwa ni sehemu muhimu ya ufanyaji kazi wa pamoja wenye lengo la kuleta maendeleo ambapo matukio mbalimbali ya AZAKI ya 2022 yatafanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 24, 2022 mpaka Oktoba 28, 2022.
“Tofauti na jitihada za awali zilizojikita katika kuelezea mchango wa sekta ya asasi za kiraia, ujumbe wa Wiki ya Asasi za Kiraia ya 2022, ambao ni ‘Maendeleo ya Watu, Simulizi za Watu’, una lengo la kuonyesha kwamba wananchi ndio washirika wetu wakubwa na sababu kubwa ya uwepo wa asasi za kiraia. Hii inaakisi hatua, mifumo na michakato mbalimbali inayotumiwa na asasi za kiraia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania, hasa zile zilizoota mizizi na za muda mrefu. Hii pia inaonyesha nia ya asasi za kiraia na washirika wa maendeleo katika kuleta maendeleo chanya na kuongoza kwa mfano,” alisema.
Wiki ya Asasi za Kiraia ni tukio muhimu la kila mwaka kwa wadau wa maendeleo nchini, ikiwa ni pamoja na Asasi za kiraia, Sekta Binafsi na Serikali kwa ujumla, kwani hao wote ni washirika muhimu wa maendeleo nchini.
Wiki hii huelekeza jitihada zake katika kuhakikisha ushiriki kamili wa washirika na wadau kutoka Sekta mbalimbali.
PICHA MBALIMBALI ZA WASHIRIKI KATIKA UZINDUZI HUO.
Social Plugin