OR-TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ameridhishwa matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya lililogharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 05, 2022 wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo hilo kwenye ziara yake ya siku Nne ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini Mbeya.
Amesema kuwa katika suala la utawala bora Serikali ya awamu ya sita inaboresha maeneo ya wananchi wanapoenda kupata huduma kuwe na mazingira mazuri ya kuhudumiwa na wale wanaotoa huduma kuweza kutoa huduma bora kwa jamii wakiwa kwenye mazingira mazuri.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kujenga majengo ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Majengo ya Halmashauri, nyumba za wakuu wa Wilaya, lengo likiwa ni kuboresha mazingira ili kuweza kutoa huduma bora kwa jamii.
“Utafiti unaonyesha kuwa tunapofanya kazi kwenye mazingira mazuri, utoaji wa huduma hutolewa vizuri hivyo Serikali imeamua kutumia fedha nyingi kujenga Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, Mheshimiwa Samia amesema Serikali itaendelea kujenga majengo kama hayo katika Mikoa yote hasa katika maeneo ya Kikanda
Mheshimiwa Samia amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo niwatake Madiwani kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ili ziweze kutekeleza miradi iliyokusudiwa na Serikali.
Jengo la Ofisi ya Mkuu w Mkoa lina urefu wa mita 84.2 na upana wa mita 33.5 ambapo vyumba vya ofisi vipo 72, stoo moja kubwa, Maktaba mbili, kumbi mbili ndogo na ukumbi mmoja mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watu 250.