JESHI LA POLISI LAFANYA UKAGUZI KWENYE MABASI YA SHULE 'SCHOOL BUS' , LABAINI MADUDU, 52 YAPEWA MAELEKEZO


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Debora Lukololo amewaagiza wamiliki na watumiaji wa magari yanayotumika kubeba wanafunzi kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Ameyasema hayo Agosti 4,2022 wakati wa ukaguzi wa magari ya shule katika Wilaya ya Shinyanga ambapo amesisitiza madereva kufuata sheria za barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti mwendo kasi ili kulinda usalama wa wanafunzi.

Afisa huyo wa jeshi la polisi amesisitiza watumiaji wa magari ya shule kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka kutumia magari mabovu ili kuepusha ajari zinazoweza kuzuilika.

”Na tutarudia kuyakagua magari yale ambayo yameonekana na makosa tuone kama yako tayari kwa ajili ya kubeba watoto tarehe za kufungua shule Mwezi wa tisa niwaombe sana wamiliki kusimamia na kuangalia tusije tukapuuza tusione kwamba Polisi wanatusumbua nikwauzima wa watoto wetu, ni kwa uzima wa madereva pia ni kwa uzima wa mali zetu kwa sababu gari linapoharibika zinaharibika mali inakuwa ngumu kuzirudisha, watoto wanapopoteza maisha ni kilio kwa wazazi, shule hata kwa Taifa inakuwa siyo vizuri pia kwenye jamii kwa hiyo niwaombe lolote lile waliloambiwa na wakaguzi wetu wa magari wahakikishe wanalirekebisha”,amesema Lukololo

Mkuu huyo wa kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Shinyanga ametaja changamoto zilizobainika kupitia ukaguzi huo uliofanyika ikiwemo baadhi ya magari kutokuwa na mikanda ya abiria pamoja na ubovu kwa baadhi ya viti ambapo amesema Agosti 25 yanatakiwa kurudishwa kwa ajili ya ukaguzi katika magari yote yaliyofunguliwa namba.

Amesema ukaguzi wa magari katika Mkoa wa Shinyanga utakuwa unafanyika baada ya miezi mitatu ambapo wiki hii jumla ya magari ya shule 52 yamekaguliwa na kupewa maelekezo.

Amewataka madereva wa magari Mkoa wa Shinyanga kuepuka mwendo kasi ili kuepuka ajari huku akiwaomba abiria kuungana kwa pamoja kupaza sauti pale dereva anapoendesha chombo cha moto bila kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kuendesha kwa mwendo kasi.

Kwa upande wake kaimu kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Leonard Nyandahu amesema zoezi la ukaguzi wa magari litakuwa endelevu ambapo amewataka madereva wanaoendesha magari mabovu kutoa taarifa sehemu husika ili wamiliki waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Nyandahu amesema lengo la ukaguzi huo ni kuimarisha usalama hasa kwa wanafunzi barabarani kuepusha ajari zinazochangiwa na ubovu wa magari pamoja na uzembe wa madereva.

Madereva wa magari yanayobeba wanafunzi wameahidi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa ili kuimarisha usalama wa wanafunzi.
Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga mrakibu mwandamizi wa Polisi Debora Lukololo wakati akizungumza na madereva
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Leonard Nyandahu wakati akizungumza na madereva




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post