HASSAN DEDE : MADEREVA TUKO TAYARI KUFANYA KAZI NA SERIKALI

 

Chama cha Madereva cha Tanzania Long Distance Trucks and Bus Association (TLDT) kimesema kiko tayari kufanya kazi na Serikali katika kupunguza vifo vitokanavyo ajali za barabarani zinazoondoa uhai wa watanzania.


Hayo yamesemwa leo Agosti 10,2022  na Mwenyekiti wa Chama hicho Hassan Dede wakati akizungumza katika kituo cha Wapo Radio kilichopo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa anaongea na jamii kuhusu shughuli na malengo ya chama hicho.


Dede amesema hizi ajali ambazo zinaonekana nchini Tanzania zingine zinatokea kwa sababu ya uzembe wa baadhi ya madereva, ulevi na zingine ni ajali ambazo zinatokana na hitilafu ya vyombo vya moto.


"Tunajua Serikali ina mawazo mazuri ya kuwalinda watu wake ila kuna hili eneo la Madereva tunaomba liangaliwe sana. Kama watatupa nafasi ya kufanya kazi na sisi tunaamini kuna adha nyingi tutapunguza" 


"Tunaomba Serikali ituamini sisi kama Chama cha Madereva (TLDT) maana kazi yetu kubwa ni kuwahudumia madereva wote pasipo na ubaguzi. Kama dereva hajapewa kazi ya udereva mwajiri wake awasiliane na chama ili apewe taarifa za huyu dereva"


"Sasa hivi kila sekta kuna chama, tunaomba kama ilivyo kwa madaktari wana chama chao, waalimu wana chama chao, wanasheria wana chama chao na sisi kama madereva tuna chama chetu cha madereva kinaitwa Tanzania Long Distance Trucks and Bus Association TLDT", alisema Hassan Dede.


Sambamba na hayo Dede amesema kuwa hawapendi kuwa kinyume na Serikali na ndio maana kila wanapotoa maelekezo, wanayapokea na kuyapa nguvu ya kutosha ili yalete matokeo mazuri kwa Madereva na makondakta pia.


Dede amefungua mlango wa madereva wote nchini Tanzania kujisajili katika chama ili taarifa zao zijulikane. Hii itasaidia kujua idadi kamili ya wanachama na kuweka mipango kamilifu ya kuwasaidia kufikia malengo yao katika sekta ya usafirishaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post