Mgeni rasmi katika Mkutano na Maonesho ya Saba ya Wahandisi Wanawake Tanzania (TAWECE), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikabidhi Cheti cha Shukrani kwa Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashanti anayeshughulikia miradi endelevu Tanzania na Ghana, Simon Shayo. Shayo alipokea cheti hicho kwa niaba ya menejimenti ya kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, waliopata tuzo hiyo kutokana na mchango wao kwa mwaka huu kwenye mkutano huouliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
**
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa wahandisi wanawake nchini hivyo wajiandae kwa fursa na ajira mbalimbali zitakazotokana na miundombinu inayojengwa kwa wingi na Serikali.
Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni katika Kongamano la Saba la Wahandisi Wanawake Tanzania (TAWECE), lililokuwa limeandaliwa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania - Kitengo cha Wanawake na kudhaminiwa na Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, kama mdhamini mkuu.
Kongamano hilo kwa mwaka huu liliongozwa na kauli Mbiu isemayo: Uajirikaji, Uongozi na Ubunifu kwa Wahandisi Wanawake Tanzania.
Majaliwa alisema, “Mpaka sasa, Tanzania tuna jumla ya wahandisi 30,921 ambapo wanawake ni 3,912 sawa na asilimia 12. Serikali imefanya uamuzi wa kujenga shule za ufundi wa kisayansi za wanawake katika kila mkoa ili kuongeza wanawake katika tasnia ya uhandisi.
Aliongeza kuwa Serikali inajenga miundombinu wezeshi kuhudumia Watanzania hivyo wahandisi wanawake wajiandae kwani fursa zipo na milango ya ajira iko wazi.
“Wanawake mnaweza na wanawake wahandisi mnaweza zaidi! Nilipata fursa ya kutembelea Daraja la Tanzanite, ambapo mhandisi aliyetoa maelezo mwanzo mpaka mwisho alikuwa mwanamke. Mji wa Serikali Dodoma, mhandisi anayesimamia ujenzi wa mradi huo unaoendeshwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ni mwanamke. Mifano ipo mingi,” alisema.
Mbali na kuwapongeza wahandisi hao wanawake kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kisarawe, alisema bado idadi ya wahandisi hairidhishi hivyo jitihada zaidi zinahitajika kuhamasisha wasichana wengi wasome masomo ya sayansi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema uhandisi kwa wanawake utaongezeka na kuimarika iwapo wahandisi wanawake wataendelea kushirikiana kuwahamasisha wenzao kujiunga kwenye uhandisi.
Naye mwenyekiti wa kitengo cha wahandisi wanawake Tanzania, Mhandisi Upendo Haule alisema wanawake ni viongozi mahiri na makini wakipewa fursa. “Tunaomba serikali iendelee kuwapa fursa wahandisi wanawake ili waendelee kuliwakilisha vyema taifa la Tanzania,” alisema Mhandisi Haule.
Baadhi ya wahandisi wanawake kutoka idara mbalimbali kwenye kampuni ya AngloGold Ashanti - Geita Gold Mining Limited pia walihudhuria Kongamano hilo na kubainisha kuwa wanawake ni viongozi mahiri na makini wakipewa fursa.
Zuhura Khamis, mhandisi wa mifumo ya kampuni aliyehudhuria hafla hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alisema ni jambo la kufurahisha kukutana na wahandisi wanawake wengi wenye vipaji.
Khamis alitaja kuwa mapenzi yake ya somo la hisabati, utatuzi wa matatizo na msukumo kutoka kwa mwalimu wake wa hisabati wa shule ya msingi ndiyo yaliyomjengea msingi wa taaluma yake kama mhandisi wa programu.
Akizungumzia kizazi kijacho cha wahandisi wanawake, Khamis alisema “Ukiwa na malengo, inawezekana kabisa ... Wasichana wasiogope kuwa wahandisi, inawezekana."
Katika kongamano hilo Waziri Mkuu alikabidhi cheti cha shukrani kwa Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, Simon Shayo na kuipongeza Kampuni hiyo kwa kwa juhudi zake za kuwezesha ustawi wa wahandisi wanawake nchini Tanzania, ikiwemo kudhamini kongamano kama mdhamini mkuu.