Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKURUGENZI KIVULINI AMPONGEZA RAIS SAMIA UJENZI WA VITUO VYA MALEZI YA WATOTO KWENYE MASOKO


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akiwa eneo la watoto kucheza katika Kituo cha Mirongo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVUNI, Yassin Ally.
Mkurgenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI la jijini Mwanza, Yassin Ally amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuagiza kujengwa kituo maalumu cha kulelea watoto katika Soko Kuu Njombe.


Ally alitoa pongezi hizo Agosti 10, 2022 baada ya Rais Samia kutoa agizo hilo kwa uongozi wa Serikali Mkoa Njombe alipokuwa akizindua soko hilo ambalo jipya lililogharimu shilingi bilioni 10.2.


Rais Samia baada ya kuzindua Soko hilo la kisasa, alisema ameona wanawake wengi wakiwa na watoto, wengine mgongoni na wengine wakicheza chini wakati mama zao wakiendelea na biashara na hivyo kuona umuhimu wa kuwa na kituo kitakachosaidia malezi ya watoto hao na kwamba wazazi wawe tayari kuchangia gharama za usimamizi.
Kufuatia maelekezo hayo ya Rais Samia, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema hatua hiyo itasaidia malezi na makuzi salama kwa watoto kipindi wazazi wao wanapokuwa kwenye biashara.


Ally alisema utafiti uliofanywa na Shirika la KIVULINI jijini Mwanza ulibaini zaidi ya asilimia 60 ya wafanyabiashara masokoni ni wanawake hivyo uwepo wa vituo vya kulelea watoto utasaidia pia kuwakinga watoto na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini pia kutoa faragha kwa wanawake wakati wa kunyonyesha.


Alisema baada ya utafiti huo, Shirika la KIVULINI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo I4IF, UKAid na IrishAid lilibuni mradi wa ujenzi wa masoko mawili ya mfano katika Hamashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela ambapo kila Halmashauri limejengwa soko moja lenye miundombinu rafiki ikiwemo vituo vya malezi na makuzi ya watoto.

"Agizo la Rais Samia limekuja wakati muafaka, Halmashauri nyingine nchini zisisubiri tena agizo lingine, zianze kujenga vituo hivi katika masoko yao na tayari vituo vya mfano viko Mwanza wanaweza kuja kujifunza" alisema Ally.


Vituo hivyo vimejengwa katika soko la Kiloleli Manisapaa ya Ilemela pamoja na soko la Mirongo jijini Mwanza ambalo mituo chake kilizinduliwa Februari 09, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima aliyesema kitasaidia malezi bora kwa watoto.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com