Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANGA JIJI YAONGOZA UKUSANYAJI MAPATO, MANISPAA YA SHINYANGA YANG'ARA, MBULU MJI BALAA, KIBAHA DC YATISHA


NA GODFREY NNKO


KATIKA kipindi cha Julai hadi Juni 2022 Halmashauri ya Jiji la Tanga imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 113 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam asilimia 108.

Huku Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa asilimia 104, Halmashauri ya jiji la Dodoma asilimia 103, Halmashauri ya Jiji la Mwanza asilimia 100 na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekua ya mwisho kwa kukusanya asilimia 92.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhesshimiwa Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Wakati huo huo, kwa upande wa halmashauri za manispaa, Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa, Manispaa ya Shinyanga imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 125 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na Ubungo asilimia 118 na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi asilimia 117.

“Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 78 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi asilimia 90 na Manispaa ya Morogoro asilimia 91,”amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Akizungumzia kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu amesema kuwa, imeongoza kwa kukusanya asilimia 140 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Mafinga asilimia 129 na Halmashauri ya Mji wa Ifakara asilimia 125.

Aidha, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 71 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri za Mji wa Korogwe asilimia 84 na Halmashauri ya Mji wa Geita asilimia 88.

Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongeza ufanisi kwani kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo imekuwa ikishika nafasi ya mwisho kwenye Halmashauri za Miji kwa kukusanya chini ya Shilingi Bilioni moja kwa mwaka.

Kwa upande wa halmashauri za wilaya, amesema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imeongoza kwa kukusanya asilimia 247 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mlele asilimia 185 na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 158.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 58 ya makisio ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe asilimia 67 ya makisio ya mwaka na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 70.

Chanzo - Dira Makini blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com