Chibalonza ana umri wa miaka 22, lakini moyo wake umetekwa na mapenzi ya babu mwenye umri wa miaka 88, Kasher Alphonse nchini Congo.
Babu huyo aliambia Afrimax English kuwa wanapendana na kuelewana licha ya tofauti ya umri wa miaka 66.
Kulingana na wapenzi hao ambao wamekuwa pamoja kwa miaka miwili, walivutiwa na nyoyo zao na wala sio miaka.
Alphonse alimuoa mke wake wa kwanza mwaka wa 1954 wakati alikuwa na umri wa miaka 24 na kujaliwa watoto saba pamoja.
Baada ya miongo kadhaa pamoja, mke wake wa ujana aliaga dunia kutokana na uzee, na kumuwacha babu huyo akiwa amevunjika moyo na mpweke kwani wanawe tayari walikuwa watu wazima na kuondoka nyumbani.
Kwa kuzingatia umri wake wa uzee, Alphonse alihangaika kujifanyia mambo mengi, hivyo akatafuta mtu ambaye angemsaida. Alikuwa na bahati kukutana na Chibalonza, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 20 lakini tayari kuwa mke wake.
"Hatujafunga ndoa rasmi lakini nimefanya naye harusi ya kitamaduni. Nilipeleka hata kreti ya bia na mbuzi aliye hai kwa familia yake," alisema.
Mzee huyo alionyesha wasiwasi kuwa hajui jinsi watoto wake watakavyoishi na mama yao wa kambo iwapo atafariki dunia.
Anajutia kuwa hana pesa za kununua kipande cha ardhi kwingine ili mke wake mchanga awe na makazi salama mbali na familia yake ya kwanza.
Watu wengi wanaojua kuhusu mapenzi huona kama ni ajabu kwa sababu watoto wote wa Alphonse ni wakubwa kuliko mama yao wa kambo, huku mwanawe wa kwanza akiwa na umri wa miaka 66, naye kitinda mimba ana umri wa miaka 50.
Alphonse anaweza kuonekana mnyonge na maskini kwa sasa, lakini anasema alikuwa akifanya vizuri kifedha katika siku zake za heri wakati huo akimiliki duka la jumla ambapo aliuza pombe.
Biashara hiyo, hata hivyo, ilifungwa baada ya msururu wa wizi ambao ulimaliza hisa zake na kufanya isiweze kuendelea.
CHANZO- Tuko News
Social Plugin