Mkuu wa idara ya Mendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Deus Mhoja, akimhoji Mtoto huyo pamoja na wazazi wake kwanini ameozeshwa katika umri mdogo.
Mtoto ambaye alikuwa akiozeshwa ndoa ya utotoni na wazazi wake akiwa ndani ya Gari la Jeshi la Polisi mara baada ya ndoa yake kutibuliwa.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wamefanikiwa kutibua Ndoa ya utotoni ambayo alikuwa akifungishwa Mtoto wa miaka 15 kwa Mahari ya Ng'ombe 10 na Pesa Taslimu Sh. 200,000/= kwa mtoto mwenzake (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 17.
Ndoa hiyo ilikuwa inafungwa Agosti 16, 2022 katika kijiji cha Manyada Kata ya Usanda Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo Askari Polisi pamoja na Maofisa hao Maendeleo ya jamii walifika eneo la tukio na kutibua ndoa hiyo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Deus Mhoja, akizungumza mara baada ya kuitibua ndoa hiyo, amesema walipata taarifa ya kufungishwa ndoa ya mtoto huyo jana kutoka kwa wasamaria wema ndipo wakapanga mikakati ya kwenda kuizuia.
Amesema Mtoto huyo (jina lake limehifadhiwa) inaelezwa amemaliza darasa la saba mwaka jana katika Shule ya Msingi Manyada, na hakuendelea na masomo, ndipo wazazi wake wakachukua maamuzi ya kumuozesha.
“Mtoto huyu sisi kama Halmashauri tutaona namna ya kumsaidia ili aendelee na masomo na kutimiza ndoto zake,kwa sababu bado ni mdogo sana na hatakiwi kuingia kwenye ndoa,”amesema Mhoja.
Naye Mama Mzazi wa Mtoto huyo (jina limehifadhiwa), amesema wamemuozesha Binti yao kwa Mahari ya Ng’ombe 10 na Pesa Taslimu Sh.200,000.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto wilaya ya Shinyanga kutoka Jeshi la Polisi Brightone Rutajama, ambaye alikuwa eneo la tukio, amesema katika Sherehe hiyo wamewakamata Bibi Harusi, Mshenga, Mama mzazi na Mjomba wake, huku wahusika wengine wakikimbia.