Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAPAN YAWATAKA VIJANA WAKE KUONGEZA KASI YA KUNYWA POMBE


Vijana wa Japani hawanywi pombe ya kutosha - jambo ambalo mamlaka zinatarajia kubadilisha kupitia kampeni mpya.


Vijana wa kizazi kipya hunywa kiasi kidogo cha pombe kuliko wazazi wao - hatua ambayo imeathiri ushuru kutoka kwa vinywaji kama sake (mvinyo unaotokana na mchele).


Kwa hivyo shirika la kitaifa linalosimamia ushuru limeingilia kati na shindano la kitaifa ili kubadilisha mawazo ya wengi .


"Sake Viva!" kampeni inatarajia kuja na mpango wa kufanya unywaji wa pombe kuvutia vijana zaidi - na kukuza sekta hiyo .


Shindano hilo linawataka vijana wenye umri wa miaka 20 hadi 39 kushiriki mawazo yao ya biashara ili kuanzisha mahitaji miongoni mwa wenzao - iwe ni kwa ajili ya Kijapani, shochu, whisky, bia au divai.


Kundi linaloendesha shindano la mamlaka ya ushuru linasema tabia mpya - ambazo ziliundwa wakati wa janga la Covid - na idadi ya watu wenye umri wa juu imesababisha kupungua kwa uuzaji wa pombe.


Inataka washindani kuja na matangazo, chapa, na hata mipango ya kisasa inayohusisha akili bandia.


Vyombo vya habari vya Japan vinasema majibu yamechanganyika, na ukosoaji fulani kuhusu jitihada ya kukuza ‘tabia mbaya’ ya unywaji pombe. Lakini wengine wamechapisha mawazo ya ajabu mtandaoni - kama vile waigizaji maarufu "wanaoigiza" kama wahudumu wa uhalisia katika vilabu vya kidijitali.


Washiriki wana hadi mwisho wa Septemba kuweka maoni yao. Mipango bora itatayarishwa kwa usaidizi kutoka kwa wataalam kabla ya mapendekezo ya mwisho kuwasilishwa mnamo Novemba.


Tovuti ya kampeni hiyo inasema soko la pombe la Japan linapungua na idadi kubwa ya watu nchini humo - pamoja na kupungua kwa viwango vya kuzaliwa - ni sababu kuu .


Takwimu za hivi majuzi kutoka kwa wakala wa ushuru zinaonyesha kuwa watu walikuwa wakinywa kiasi kidogo cha pombe mnamo 2020 kuliko 1995, na idadi hiyo ilishuka kutoka lita 100 (galoni 22) kwa wiki hadi lita 75 (galoni 16).


Mapato ya ushuru kutoka kwa ushuru wa pombe pia yamepungua kwa miaka ya hivi karibuni. Kulingana na gazeti la The Japan Times, iliunda 5% ya mapato yote mnamo 1980, lakini mnamo 2020 mapato yalifika 1.7%.


Benki ya Dunia inakadiria kuwa karibu theluthi moja (29%) ya wakazi wa Japani wana umri wa miaka 65 na zaidi - idadi kubwa zaidi duniani.


Wasiwasi juu ya mustakabali pombe ya ‘sake’ sio shida pekee ambayo inayotishia uchumi wa Japani - kuna wasiwasi juu ya usambazaji wa wafanyikazi wachanga kwa aina fulani za kazi, na utunzaji wa wazee katika siku zijazo.

Via >> BBC SWAHILI


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com