Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar [SMZ], kupitia kwa Mkuu wake wa Wilaya ya Mjini Mh.Rashid Simai Msaraka imesema inatambua na juhudi za tamasha la Reggae Zanzibar katika kuleta tija ya kukuza uchumi Visiwani Zanzibar.
Mh.Msaraka amesema hayo katika mkutano maalum wa Waandisshi wa Habari na Wasanii wa Reggae wanaoshiriki msimu wa Nne wa tamasha la Muziki wa Rege [Zanzibar Reggae Festival] linalofanyika kwa siku mbili Agosti 5-6, ndani ya Mambo Club, Mji Mkongwe.
‘’Serikali inatambua umuhimu wa matamasha ya muziki ndani ya Zanzibar, pia mziki wa Reggae tunataka uwe mkubwa na kuendelezwa kama Sera ya Serikali na Chama chetu cha Mapinduzi [CCM] sababu yanaleta tija katika uchumi na kukuza ajira kwa vijana na jamii kwa ujumla, na kuongeza kuwa, wanaamini Tamasha hilo litakuwa kubwa na miongoni mwa matamasha yatakayochangia uchumi Visiwani hapa", alisema Mh. Msarika
Aidha, amewataka Watu waachane na imani potofu kwa jamii ya Kirasta na muziki wa Reggae, kwani ni kama imani nyingine, zaidi amewataka kuzingatia sheria za nchi zilizopo.
Hata hivyo, amewataka watu wenye imani ya Kirasta kusaidiana na Serikali kufichua wanaotumia jina la ‘RASTA’ vibaya kama kuiba, kubaka ama kufanya uhalifu hali inayopelekea taswira mbaya kwa jamii na Serikali.
"Naomba tuendelee kuwa wa mfano, ikiwemo kushirikiana na Serikali, kakatika kufichua masuala ya kialifu, tukemeane wenyewe kwa wenyewe, ili kulinda imani hii na sisi Serikali milango iko wazi kuendelea kushirikiana.
..Watu wanaotaka kujua mengi kuhusu Rasta waweze kujiunga na Rasta wenyewe, ambao Wana umoja wao, kwani pia wanaubiria amani na upendo", Alisema Mhe. Msaraka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Said Omary Hamad ‘Side Rasta’ ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono uwepo wa tamasha hilo huku akiomba wadau mbali mbali waendelee kujitokeza kudhamini.
"Tunaomba wadau mbali mbali kujitokeza kudhamini tamasha la Reggae Zanzibar, kwani uwepo wa tamasha ni ukuaji wa uchumi wetu, milango ya udhamini ipo wazi’’, alieleza Side Rasta.
Aidha, amewataja Wasanii wa muziki wa Reggae kwenye tamasha hilo kuwa ni Ras Gumbo, Nile Dawta (Nairobi Kenya), Mr Kamanzi, Mack El Sambo (DRC Congo), Brasto Imva (Malawi ), Ras Coco (Zanzibar) na Zion Rebels (Ethiopia) na wengineo.