Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi za kimataifa, Tanzania inashika nafasi ya sita kwa Bara la Afrika kwa kuwa na gharama za chini za bando “vifurushi” huku ikishika nafasi ya 32 Duniani kwa gharama ya chini ya data.
Waziri Nape ametoa ufafanuzi huo wakati aliposhiriki kipindi cha Power
Breakfast on Saturday cha Clouds TV na redio, leo Agosti 20, 2022 jijini
Dar es Salaam ambapo amesema bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola 1.71 sawa na
shilingi 3990.
“Tanzania kuwa miongoni mwa Mataifa yenye gharama za chini za mawasiliano
haimaanishi kuwa itapunguza malalamiko kwa kuwa uchumi wetu haufanani na
wananchi wengi wana kipato cha chini”, amesema Waziri huyo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imeendelea kufanya tathmini ya gharama za uwekezaji, utunzaji na usafirishaji
wa data kila baada ya miaka minne na tathmini nyingine inafanyika mwaka huu ili
kupata uhalisia wa gharama za bando kama zitapanda au kushuka.
“Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa Serikali yao ni sikivu na inafanyia
kazi malalamiko na maoni ya wananchi, lakini pia nitoe rai kwa wananchi kuwa makini
na matumizi ya simu janja hasa kwenye kujiunga na huduma mbalimbali pamoja na programu tumizi “applications” ili kupunguza matumizi ya bando”, amesisitiza Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape amesema kuwa Serikali imeruhusu ushindani kwa kuweka
mazingira wezeshi ya kuwa na kampuni nyingi zinazotoa huduma za mawasiliano ambapo
huduma ya vifurushi ni huduma ya ziada inayotolewa na makampuni hayo na kuleta
unafuu wa gharama za mawasiliano.
Ameongeza kuwa kwa
ulimwengu wa sasa wa kidijiti huduma nyingi zinapatikana kwa njia ya mtandao,
hivyo kuifanya huduma ya intaneti kuwa huduma muhimu na ya msingi katika
kuendesha shughuli za uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine Waziri Nape ameielekeza TCRA, Baraza la Watumiaji
wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) na Makampuni ya simu kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi na kujibu au kutoa ufafanuzi wa maswali na malalamiko ya wananchi
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Social Plugin