Na Dotto Kwilasa, DODOMA
WIZARA ya uwekezaji,viwanda na biashara kupitia kituo chake cha uwekezaji (TIC) imesema inaendelea na kutambua wa fursa za uwekezaji,kutangaza fursa za uwekezaji,kusajili miradi ya uwekezaji ,kusaidia upatikanaji wa vibali na leseni kwa wawekezaji ili kukuza uchumi wa nchi.
Kaimu Meneja wa kituo hicho kanda ya kati Juma Nzima amesema hayo leo jijini hapa katika maonesho ya nane nane,Kanda ya kati na kueleza kuwa ili kufanikisha uwekezaji nchini kituo hicho kinasimamia upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji na kutatua changamoto za uwekezaji.
Amesema TIC kama kituo cha uwekezaji kinahakikisha kinawavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza sekta binafsi na hatimaye kuinua uchumi wa taifa ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali juu ya maswali yanayohisu uwekezaji nchini.
Pamoja na hayo Kaimu Meneja huyo wa TIC amesema kituo hicho kimejikita katika kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa ambayo inakenga Tanzania kuwa ya viwanda ifikapo 2025.
"Kazi zinazofanywa na kituo hiki ni kuhakikisha tunafanikisha kufanya tafiti zenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji kwa wajasiriamali na kufanikisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji inayoanzishwa ,"amesema
Akieleza taratibu mbalimbali za huduma kwa wawekezaji Nzima amesema ili wawekezaji waweze kuanzisha miradi mbalimbali nchini wanahitaji kupata vibali na leseni kupitia kitengo Cha huduma za mahala pamoja na kwamba utaratibu wa kupata cheti cha uwekezaji unazingatia uthibitisho wa fedha za kutosha za kutekeleza miradi.
"Kuna masharti pia katika utaratibu wa usajili wa Kampuni za nje ambapo mwekezaji atatakiwa kuwasilisha nyaraka tatu kutoka kwenye kampuni mama ambazo zimethibitishwa na mwanasheria wao ambazo ni katiba ya Kampuni,cheti cha usajili wa Kampuni na taarifa za ukaguzi wa mahesabu,"amefafanua
Sambamba na hayo ameeleza kuwa kupitia maonyesho hayo nanenane,wanatumia kama fursa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utaratibu wa kuomba leseni ya biashara Kwa ajili ya uwekezaji ambapo mwombaji ataambatanisha nakala ya cheti cha Kampuni Kwa wale wenye makampuni au cheti cha usajili Kwa wenye majina ya kibiashara.