Picha haihusiani na habari hapa chini
Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Kabula Ngasa mwenye umri wa miaka 60, mkazi wa kijiji cha Nyida Kata ya Nyida katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga , ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyida Kidoto Maganga ameiambia Redio Faraja kuwa, tukio hilo limetokea majira ya saa tatu usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 1,2022, wakati Marehemu akiwa nyumbani kwake katika kijiji hicho.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa, watu waliofanya mauaji hayo walikuwa ni wawili ambao walifika nyumbani kwa Marehemu mapema na kujifanya wateja katika kibanda chake cha bidhaa ndogo ndogo kilichopo hatua chache kutoka kwenye nyumba yake ambapo mwanzoni waliagiza Pipi na baadaye Soda na kuhudumiwa.
Baada ya dakika chache kupita walimtuma mjukuu wake anayesoma darasa la nne aliyekuwa naye kibandani kuwafuatia maji ya kunywa ndani, ambapo baada ya kurudi na maji walimpiga kwa ubapa wa panga hali iliyosababisha aanguke chini.
Alipoamka alikimbia kwa Mama yake ambaye anaishi jirani na kumweleza kinachoendelea, lakini inaelezwa kuwa Mama wa mtoto huyo aliogopa kutoka nje kwa vile Mume wake hakuwepo na hivyo watu hao wakatumia mwanya huo kumshambulia marehemu kwa Panga sehemu mbalimbali za mwili wake mpaka alipofariki dunia.
Diwani wa kata ya Nyida Selemani Seregeti , amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga George Kyando akibanisha kuwa,bado hajapata taarifa za tukio hilo kwa sababu yuko nje ya ofisi kikazi.
Social Plugin