Ayman al- Zawahiri akiwa na aliyekuwa Kiongozi wa kundi la Al-Qaeda Osama Bin Laden
Ayman al-Zawahiri aliyekuwa kiongozi wa kundi la lkigaidi la Al- Qaeda
***
RAIS wa Marekani Joe Biden amelihutubia Taifa hilo na kutoa kauli nzito juu ya kifo cha kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda Ayman al-Zawahiri, aliyeuawa na ndege ya Marekani isiyokuwa na Rubani.
Rais Biden amesema kuwa kifo cha al- Zawahiri ni malipo ya unyama alioufanya kwa wananchi wa Taifa hilo kufuatia kuhusika katika utekelezaji wa shambuliola kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 ambalo liliua zaidi ya raia 3000 nchini humo.
Rais wa Marekani Joe Biden
“Kiongozi wa ugaidi hayupo tena.” Alinukuliwa akisema Rais Biden ambaye aliendelea kwa kusisitiza kuwa kifo cha gaidi huyo kinarudisha tena faraja kwa familia za wahanga wa shambulio la Septemba 11.
Rais huyo wa Marekani amesisitiza kuwa Afghanistan haitakuwa tena makazi ya ugaidi baada ya shambulio hilo kutekelezwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu vikosi vya Marekani vindoke nchini humo.
Aidha kiongozi huyo wa kundi la kigaidi ambaye ana asili ya Misri aliuawa majira ya asubuhi wakati akiwa katika nyumba yake kwenye mji wa Kabul ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais Biden ni kwamba hakuna mtu mwingine yeyote yule kutoka katika familia ya al- Zawahiri aliyeathirika au kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Al-Zawahiri aliuawa vipi?
Maafisa wa Marekani wamesema Zawahiri alikuwa amesimama kwenye veranda ya nyumba yake ya mafichoni. Ghafla, ndege isiyokuwa na rubani- inayofahamika kama drone- ikadondosha makombora mawili.
Taarifa inasema kuwa kombora lilimpiga Zawahiri ambaye alikuwa amesimama nyumbani kwake.
Ndugu wengine wa familia ya Ayman Al-Zawahiri walikuwepo pamoja naye katika eneo hilo, lakini hakuna mtu mwingine aliyeuawa wala kujeruhiwa katika shambulio hilo, na kiongozi wa Al-Qaeda akafa mara moja pale peke yake, maafisa walisema.