Mwanamke mmoja mkazi wa mtaa wa Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga anayejulikana kwa jina la Hawa Hussein amelazwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa maji ya moto na mpangaji mwenzake.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kambarage Bwana Marik Juma ameiambia Redio Faraja kuwa tukio hilo limetokea saa tatu usiku wa kuamkia leo Jumanne Agosti 2,2022, na alipewa taarifa kwa njia ya simu na Wasamaria wema.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo aliwasiliana na viongozi wenzake ikiwemo wale wa jeshi la jadi Sungusungu ambapo waligawanyika na baadhi walimchukua majeruhi na kumpeleka katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa matibabu na wengine na wengine walimchukua mtuhumiwa na kumpeleka Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria.
Majeruhi ameunguzwa sehemu ya mbele ya mwili wake na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Redio Faraja imefika katika Hospitalini hapo na kuzungumza na majeruhi ambapo ameeleza kuwa, hafahamu sababu za kufanyiwa kitendo hicho na kwamba, alikuwa akisikia maneno yasiyokuwa mazuri yakizungumzwa na jirani yake huyo kuhusu maisha yake, lakini alichukulia kama ni jambo la kawaida.
Baadhi ya wapangaji walioshuhudia tukio hilo wamebainisha kuwa,walimuona mtuhumiwa akimwagia maji ya moto mwenzake mara tu alipotoka nje kukata Karoti kwa ajili kufanya maandalizi ya chakula cha usiku.
CHANZO - RADIO FARAJA BLOG
Social Plugin