Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU WA CCM DANIEL CHONGOLO ATOA MAELEKEZO 10 SERIKALINI AKIHITIMISHA ZIARA KILIMANJARO

 


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amehitimisha ziara ya siku nne mkoani Kilimanjaro, katika Wilaya ya Same,  Jumamosi, Agosti 6, 2022, ambapo katika ziara hiyo pamoja na kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi, Uhai na uimara wa Chama ngazi za mashina, pia ametoa maelekezo mbalimbali kwa serikali na wananchi ili kuhakikisha utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025 inatekelezwa kwa ufanisi.

STENDI YA NGANGAMFUMANI: Akizungumzia stendi hiyo ya kimkakati ya mabasi Ndugu Chongolo, ameziagiza wizara mbili, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Fedha, kukamilisha ujenzi huo haraka iwezekanavyo.

Stendi hiyo ambayo inatarajiwa kugharimu Sh. 17 bilioni hadi itakapokamilika, ilianza kujengwa mwaka 2018 na ilitakiwa ikamilike mwaka 2020 ambapo tayari zimeshatumika Sh. 7 bilioni, hivyo bado Sh. 10 bilioni kwa sasa ili kuimalizia.

SOKO LA MANYEMA: Katibu mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Rashid Gembe, kufanya tathmini ya kuandaa michoro ya Soko la Manyema, ili liweze kujengewa miundombinu na wafanyabiashara wa samaki wabichi, warudi katika soko hilo, watoke Soko la Pasua walikohamishiwa.

"Mkuu wa Wilaya, wewe ndiye kamisaa hapa, simamia ndani ya wiki moja, wataalamu wafanye tathmini ya eneo hilo, kama linafaa kwa ajili ya biashara, wachore michoro kwa ajili ya miundombinu ya soko hilo, baada ya wiki moja nategemea taarifa itakuwa imekamilika na utaniletea ili sisi tusaidie kusukuma hiyo fedha ya kujenga soko katika eneo hilo la Manyema ipatikane,” amesema Katibu Mkuu.

MABALOZI: Vilevile Katibu Mkuu ameagiza miradi yote itakayotekelezwa kwenye jamii, iwe imeibuliwa kutoka ngazi za chini za mabalozi, kwenye vikao vya mashina.

"Msipitishe miradi bila kuwaalika mabalozi wa maeneo husika, mkiwaalika mabalozi wakija mtajadiliana na kufikia maamuzi ya miradi iwekwe wapi kwenye mahitaji halisi ya wananchi, miradi iibuliwe kutokea ngazi ya chini na ngazi ya msingi ianze kwenye mashina.”

UPIMAJI MAENEO YA UMMA: Katika ziara hiyo pia Katibu Mkuu ameziagiza Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Nyumba na Makazi kuweka mpango na kipaumbele katika kupima maeneo yote ya umma, yanayotoa huduma za jamii, nchi nzima na kuhakikisha yanakuwa na hati miliki.

"Ni lazima Tamisemi waweke programu ya kupima maeneo yote na kuweka malengo kwa kila mkurugenzi na katibu tawala wa mkoa kuhakikisha kwa kipindi fulani wanayatambua maeneo yote ya umma na kuyapima kisheria, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima katika kujihakikishia umiliki wa maeneo hayo.”

UCHELEWESHAJI WA MIRADI:
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo pia ameagiza kasi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Whona-Marangu-Omboni uliopo Wilaya ya Rombo na ule wa Same-Mwanga-Korogwe, kuongezwa ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi katika maeneo hayo.

Amewataka Wizara ya Maji, kufanya kazi kwa bidii ili kutafsiri katika matokeo maelekezo yaliyoko katika Ilani na maagizo ya Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Samia Suluhu Hassan. Katibu Mkuu amesema Chama hakitawakalia kimya wote wasiotimiza wajibu wao kutatua changamoto za Watanzania, kwani huko ni sawa na kukigombanisha chama na Mwenyekiti wake kwa wananchi.

UMEME
Katibu Mkuu amesisitiza bei ya umeme kwa maeneo ya vijijini ni sh 27,000 na nguzo ni bure, hivyo kuagiza Wizara ya Nishati kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) kuharakisha uwekaji umeme kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa shughuli za uchum na kujipatia kipato.

BARABARA Katibu Mkuu amesema kuwa hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Barabara ya Mwanga-Kikweni- Vuchama na kuagiza mamlaka zinazohusika kusimamia ujenzi huo, kuanza kumkata fedha mkandarasi anayejenga kipande cha kilometa 1.2 kwa kiwango cha lami, endapo atashindwa kukamilisha ujenzi huo ifikapo Agosti 8, mwaka huu, kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo.

"Wao sisi tukiwacheleweshea mahitaji yao huwa wanatupa adhabu sasa kwa sababu katika mradi huu sisi hatujachelewesha ni wao wamezembea wapewe adhabu na adhabu hiyo isiwe kigezo cha kuendelea kuuchelewesha huu mradi bali iwe kigezo cha kuukamilisha haraka. Na iwe fundisho kwa wakandarasi wengine pia.”

CHAKULA: Katibu Mkuu amewataka wananchi kutumia vizuri na kutunza chakula walicho nacho, na wale wenye mifugo mingi kuipunguza kwa kuiuza na kununua chakula ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chakula ambao imetokana na uhaba wa mvua za kutosha kwa msimu wa kilimo 2021/2022.

UKOSEFU WA DAWA: Aidha Katibu Mkuu amesikitishwa na kitendo cha wananchi kukosa huduma ya dawa katika zahanati wilayani Mwanga, kutokana na deni la Sh 104 milioni, wanalodaiwa na Bohari ya Madawa nchini (MSD).

"Kwa kweli nimesikitishwa kusikia dawa haziji eti kwa sababu kuna deni, hiyo haikubaliki na hiyo siyo sawa, ni lazima tujue kama kuna changamoto tutafute njia ya kuitatua lakini sio kusitisha huduma kwa wananchi, tunakwenda kubanana huko, kujua changamoto ya hayo madeni kwenye zahanati na tujue yako kwa kiwango gani, ili kutafuta ufumbuzi wa haraka katika maeneo yote nchini.”

UTALII: Aidha Katibu Mkuu pia amewataka wananchi kutumia fursa ya utalii iliyopo kwa sasa ambayo imepewa hamasa kubwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mkakati wa Filamu ya TANZANIA, THE ROYAL TOUR, kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kujiongezea kipato na kunufaika kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com